Nuru FM
Nuru FM
23 March 2026, 12:00 pm

Wanahabari Mkoani Iringa wametakiwa kutumia mafunzo hayo vizuri katika kuripoti masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabia ya Nchi.
Na Telesia Chalamila
Waandishi wa habari 20 kutoka vyombo mbalimbali mkoani Iringa wamepatiwa mafunzo maalum yanayozingatia masuala ya kijinsia na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni juhudi za kuongeza uelewa katika kuripoti athari za mabadiliko hayo kwa jamii.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, mkufunzi kutoka TGNP, Deogratius Temba, amesema lengo ni kuhakikisha waandishi wa habari wanatoa nafasi kwa sauti za makundi yakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema ni muhimu kwa waandishi hao kuzingatia usawa wa kijinsia katika uandishi wao ili kuibua changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kusaidia kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TGNP kwa kuwapatia elimu hiyo, wakiahidi kuitumia kuboresha kazi zao za kila siku kwa kuzingatia masuala ya kijinsia wanaporipoti habari mbalimbali.
Mradi huo wa HROP Resilience unaendelea kutekelezwa katika mkoa wa Iringa, hususan katika halmashauri za Wilaya ya Iringa, Kilolo na Mufindi, ukiwa na lengo la kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
