Nuru FM

Serikali yawekeza bilioni 59 kukuza utalii Ruaha

11 February 2026, 9:51 am

Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika Picha ya pamoja na watumishi wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Picha na Ayoub Sanga

Mradi wa REGROW unalenga kuimarisha sekta ya utalii, kulinda rasilimali asilia na kukuza uchumi wa Mkoa wa Iringa.

Na Hafidh Ally

Mradi wa uboreshaji wa usimamizi wa maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wenye thamani ya Shilingi bilioni 59 unaotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha mkoani Iringa unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya utalii kwa kuimarisha miundombinu.

Akizungumza baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Kheri James amesema kupitia mradi huo utasidia kuongeza idadi ya watalii na kukuza utalii wenye tija kusini mwa Tanzania.

Sauti ya RC Kheri

Amesema mradi huo umejikita katika kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa viwanja viwili vikubwa vya ndege ndani ya hifadhi, maeneo ya malazi yakiwemo hosteli, pamoja na ujenzi wa kituo maalum kwa ajili ya watafiti na waikolojia watakaofanya tafiti mbalimbali katika hifadhi hiyo.

Sauti ya RC Kheri

Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Emmanuel Moirana, amesema mradi huo utaongeza vivutio vya utalii, kuimarisha huduma muhimu kwa watalii, na kuchochea ukuaji wa utalii Mkoani Iringa na Kusini mwa Tanzania kwa ujumla.

Sauti ya Mkuu wa Hifadhi

Naye Afisa Mhifadhi Mkuu na Msimamizi wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Amina Salum, amesema kuwa miradi hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika kuimarisha utalii wa ndani akibainisha kuwa malazi yameboreshwa na idadi ya vitanda imeongezeka, ambapo jumla ya vitanda 158 vimeongezwa pamoja na ujenzi wa hostel yenye uwezo wa kuchukua wageni 126.