Nuru FM
Nuru FM
24 October 2025, 8:34 am

“Magari haya yatakuwa chachu ya kupunguza matukio ya uhalifu mkoani Iringa”
Na Hafidh Ally
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amekabidhi magari mapya manane (8) kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuimarisha ulinzi na usalama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa Kheri James alisema magari hayo yatatumika katika shughuli zote za kipolisi mkoani humo, ikiwemo doria, ufuatiliaji wa matukio ya uhalifu na utoaji huduma kwa wananchi kwa haraka zaidi.
RC Kheri James amesema magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya serikali ya kuimarisha usalama wa nchi, hasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Octoba 29 2025.

Aidha RC Kheri James ameagiza magari hayo yatunzwe na yatumike kwa maslahi ya uma na shughuli za kipolisi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia magari hayo kwani yatachangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu.
Awali, akisoma taarifa ya magari hayo, ofisa wa polisi, Eustace Kinuno ameeleza kuwa magari yaliyotolewa ni Toyota Land Cruiser GXR 300, Toyota LX 5D Pick Up (2), Toyota LX 5D Hard top (2) na Toyota Hillux Double Cabin (3) huku akisema lengo ni kuleta mapinduzi katika kuimarisha doria na usalama wa raia.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Iringa, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, makamanda wa polisi, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi.