Nuru FM
Nuru FM
21 October 2025, 11:07 am

“Magari haya yatasaidia kupunguza majanga ya moto katika jamii” RC Kheri
Na Hafidh Ally
Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amekabidhi rasmi magari na vitendea kazi vya kisasa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuimarisha utendaji wa Jeshi hilo katika kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoweza kutokea katika jamii.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo Komred Kheri James ameeleza kuwa lengo la kukabidhi vifaa hivyo ni kuwa na majeshi imara yenye askari wenye nidhamu, utiii na vifaa vinavyo weza kutoa huduma bora kwa raia na mali zao.

Aidha RC amebainisha kuwa Mkoa wa Iringa umepokea magari tisa yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za aina yoyote inayotokea katika jamii, na vifaa vya kisasa vya kurahisisha uokoaji na kulinda usalama wa waokoaji.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Jackline Mtei, amesema ujio wa magari hayo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa jeshi hilo katika kushughulikia matukio ya moto na uokoaji ndani ya mkoa.
Nao wananchi Manispaa ya Iringa wameishukuru serikali kwa kulwezesha jeshi hilo kupata magari hayo ambayo yatasaidia kukabiliana na matukio ya moto katika jamii.