Nuru FM
Nuru FM
14 October 2025, 9:48 am

Kukamilika kwa ujenzi wa Soko la Machinga Complex Iringa utarasihisha wajasiriamali kufanya kazi zao kwa uhuru.
Na Adelphina Kutika
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Soko la Machinga Complex kutakuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wadogo katika Manispaa ya Iringa.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni Uliofanyika kata ya Ilala, Ngajilo amesema mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipita mkoani Iringa kuomba kura na kuahidi kukamilisha ujenzi wa soko hilo, ambalo sasa linatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wamachinga.

Aidha Ngajilo, ameahidi kushirikiana kwa karibu na Serikali kuhakikisha kero zinazowakabili wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iringa (Frelimo) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa zinapatiwa suluhisho la kudumu ili wananchi wapate matibabu bora, yenye staha na kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Iringa Mjini, Isack Kikoti, amewataka vijana wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi na kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao.