Nuru FM

Kituo cha polisi Tanangozi suluhu ya uhalifu

30 August 2025, 10:30 am

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa Ikiongozwa na RC Kheri James wakati wa uzinduzi wa kituo cha Polisi Tanangozi. Picha na Ayoub Sanga

Kabla ya kituo hicho kujengwa wananchi walikuwa wakijichukulia sheria mkononi jambo ambalo kwa sasa halikubaliki.

Na Godefrey Mengele

Wananchi wa kijiji cha Tanangozi kata ya Mseke halmashauri ya wilaya ya Iringa wametakiwa kutumia kituo kipya cha polisi kuripoti matukio ya kihalifu na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Akizundua kituo hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ili kutokomeza matukio mbalimbali ya kihalifu huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali hasa wenyeji wa Mkoa wa Iringa wanaoishi Mikoa mingine kuwa na muamko wa kukumbuka kurudisha fadhira ya maendeleo katika maeneo wanayotoka.

Sauti ya RC Iringa

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amesema kuwa awali wananchi katika eneo hilo walikuwa wanapata huduma za kipolisi nje ya eneo hilo hivyo uwepo wa kituo hicho utasaidia kuthibiti uhalifu na wahalifu na kuonya tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Sauti ya RC Iringa

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi ametoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Tanangozi kilichopo Kata ya Mseke Wilaya ya Iiringa kutojihusisha na vitendo vya kuwalinda au kuwaficha wahalifu.

Sauti ya Kamanda

Kwa upande wake Mdau wa maendeleo aliyefanikisha kujengwa kwa kituo hicho Safiani Mgunda pamoja na wananchi wa wamesema eneo hilo lilikuwa na uhitaji mkubwa wa kujengwa kwa kituo hicho ili kudhibiti matukio yaliyokuwa yanatokea mara kwa mara ikiwamo ajali.

Sauti ya Mdau Mgunda

Kituo cha Polisi tanangozi ni cha Daraja C na ujenzi wake umegharimu shilingi milion 58 kikielezwa kuwa hakitasaidia usalama pekee bali pia fursa ya kukuza maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Tanangozi kwani mazingira salama huwezesha shughuli za kibiashara na uwekezaji kustawi.