Nuru FM

RUWASA Iringa yatakiwa kusimamia Miradi ya Maji

5 August 2025, 9:40 am

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Bi. Nuru Nsovera akizungumza na Watumishi wa Ruwasa. Picha na Ayoub Sanga

Usimamizi wa Miradi ya Maji sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya majisafi, salama na ya uhakika.

Na Ayoub Sanga

Watumishi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wametakiwa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi miradi ya maji inayofadhiliwa na Serikali, kwa kuhakikisha inasimamiwa kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa, ili kufanikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi hususani vijijini.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Bi. Nuru Nsovera, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa, katika kikao kazi maalum cha watumishi wa RUWASA kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa lengo la kujadili mafanikio, changamoto na kupanga mikakati ya kuboresha huduma za maji katika mwaka ujao wa fedha.

Bi. Nsovera amewataka watumishi hao kuwa na uwajibikaji wa hali ya juu katika utekelezaji wa miradi, akisisitiza kuwa miradi ya maji ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa ajili ya kuinua hali ya maisha ya wananchi.

Sauti ya RAS

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Iringa Mhandisi William Tupa, amesema kikao hicho kimekuwa jukwaa muhimu kwao kama taasisi kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka uliopita wa fedha, pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha huduma za maji zinaboreshwa zaidi.

Sauti ya Meneja RUWASA

Naye mmoja wa watumishi waliokuwa miongoni mwa washiriki wa kikao hicho, Bi. Hilda Mnyawami, amesema kikao hicho kimetoa maarifa na mwelekeo mpya kwa watendaji wa RUWASA.

Sauti ya Hilda

Kupitia kikao kazi hicho, RUWASA Mkoa wa Iringa imeazimia kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi, kuongeza uwazi katika matumizi ya rasilimali, na kuimarisha ushirikiano kati ya watendaji na jamii husika ili kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi.