Nuru FM

Jesca awachangia milion 5 waathirika wa moto

15 July 2025, 12:31 pm

Jesca Msambatavangu akikabidhi fedha kwa kiongozi wa soko Mashine tatu. Picha na Ayoub Sanga

“Fedha hizi zitawasaidia wafanyabiashara wa soko la Mashine tatu na kuanza upya biashara kutokana na madhara ya moto” Jesca

Na Hafidh Ally

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza Muda wake Jesca Msambatavangu, ameanzisha Mfuko Maalum wa Msaada kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara walioathirika na janga la moto katika soko la Mashine Tatu na tayari amechangia kiasi cha Sh milioni tano.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mh. Jesca amesema anaelewa uchungu na mateso yanayowakabili wafanyabiashara hao, huku akiwasihi kutokata tamaa na badala yake kuendelea kuwa na matumaini.

“Najua jinsi mlivyopambana kujenga biashara zenu. Hili ni pigo kubwa, lakini si mwisho wa kila kitu. Tumuombe Mungu na tusonge mbele,” amesema.

Sauti ya Jesca

Aidha, Jesca alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara hao kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kuweka mazingira sawa ili kuwawezesha wahanga hao kurejea katika shughuli zao za kujipatia kipato.

Sauti ya Jesca

Aidha, Jesca alitumia fursa hiyo kuhamasisha mashirika ya kiraia, taasisi za dini, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kuchangia katika mfuko huo kwa moyo wa uzalendo, ili kuwawezesha wahanga hao kurejea katika shughuli zao za kujipatia kipato.

Naye Mwenyekiti wa Soko la Mashine Tatu Japhar Sewando Osama amemshukuru Jesca Msambatavangu kwa msaada huo huku wakiishukuru Bakwata ambao ndio wamiliki wa eneo la soko hilo kwa kukubali kufanya marekebisho ili waendelee na biashara zao.

Sauti ya Osama

Moto huo mkubwa uliotokea hivi karibuni umeripotiwa kuathiri zaidi ya wafanyabiashara 500, wakiwemo 450 waliokuwa ndani ya soko hilo na wengine 85 waliokuwa wakifanya biashara katika vibanda vya nje na kuacha maumivu makubwa ya kiuchumi kwa familia nyingi, huku thamani ya mali zilizoteketea ikikadiriwa kufikia mamilioni ya shilingi.