

19 February 2025, 10:43 am
Na Victor Meena
Wananchi wa Kitongoji cha Imalinyi kilichopo Kijiji cha Lupembelwasenga Kata ya Lyamgungwe Mkoani Iringa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji jambo linalohatarisha usalama kwao.
Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa wanatumia maji yasiyo safi na salama ya kwenye mabonde na wanafunzi wengine kufuata maji mbali jambo linalopelekea washuke kitaaluma.
Aidha wananchi hao wameiomba serikali kuwapatia huduma ya maji licha ya awali kuwa na mradi wa maji ambao kwa sasa haufanyi kazi kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM Kijiji cha Lupembelwasenga Salum Kisoli amesema kuwa kulikuwa na changamoto ya mota kuharibika katika matenki ya maji lakini tayari wamesharekebisha na maji yatanza kutoka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupembelwasenga Bw. Ezekiel Muhehe alishindwa kujibu jinsi gani watatatua kero ya Maji kwa wananchi wake.
MWISHO