Manispaa ya Iringa yatoa mkopo wa mil. 528.7 kwa vijana wanawake na wenye ulemavu
20 January 2025, 11:38 am
Na Godfrey Mengele
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeanza rasmi zoezi la utoaji mikopo kwa wanufaika 52 wa vikundi vya Vijana, Wanawake na wenye Ulemavu, vilivyo kidhi vigezo vya kupewa Mikopo hiyo, kwa kupewa hundi ya kiasi cha shilingi Milioni 528.76 ili kuwawezesha Wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Iringa, Kheri James, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kutimiza wajibu huo wa kisheria wenye lengo la kuinua hali za kiuchumi za wananchi hasa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.
DC Kheri James ameeleza kuwa lengo la utoaji wa mikopo hiyo ni kuunga mkono juhudi za Wananchi katika shughuli zao za uzalishaji mali, Kuongeza mnyororo wa thamani, kutengeneza ajira, kukuza biashara na kuchochea upatikanaji wa huduma katika jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa Mkopo Huo Manispaa ya Iringa wamesema kuwa utawasaidia katika utekelezaji wa shughuli zao za kiuchumi huku wakiahidi kurejesha kwa wakati ili wengine wanufaike.
Serikali wilayani Iringa tayari imefanikiwa kutoa mikopo katika Halmashauri zake mbili na inaendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo Wananchi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.
MWISHO