Nuru FM

Shamba la SAOHIL kuwa chachu ya Uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki

12 January 2025, 12:08 pm

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo akiwapokea viongozi mbalimbali.

Na Mwandishi wetu

Shamba la Miti Sao Hill lililo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania limetajwa kuwa chachu ya uhifadhi wa rasilimali misitu na nyuki hususani katika wilaya ya Mufindi kutoka na shughuli mbalimbali zinazofanyika na shamba katika sekta ya misitu na nyuki.

Akizungumza kuelekea ziara ya mafunzo inayotarajia kufanywa na viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura amesema kuwa lengo ziara hiyo ni kuona namna gani Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imefanikiwa katika shughuli za uhifadhi zinazochagizwa na uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill.

“Shughuli za uzalishaji wa mazao ya misitu umechangia kuwepo kwa maendeleo katika Wilaya ya Mufindi kwani mapato mengi yanakusanywa kupitia kodi zinazolipwa hivyo tumekuja kuona na kujifunza kwa namna gani sisi pia tutanufaika na uwepo wa shamba la Miti Silayo”

Akizungumza wakati wa mapokezi ya vuongozi hao, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo amesema Shamba la Miti Sao Hill limekuwa mfano mzuri wa uhifadhi hususani katika uanzishaji wa mashamba ya miti katika maeneo mbalimbali nchini kwani manufaa na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kimazingira yamekuwa chachu katika maendeleo ya maeneo mengine.

Aidha ameongeza kuwa uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill umekuwa na mchango mkubwa katika uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha mazao ya misitu kutokana na uwepo wa malighafi zinazotumika kuzalisha mazao hayo na kuchangia ukuaji wa mapato ya halmashauri za Wilaya, Mkoa na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mufindi Ndg. Reuben Chongolo amesema kuwa viongozi hqo kutoka Wilaya ya Chato kupitia ziara hiyo watatembelea katika eneo la shamba la Miti Sao Hill kuona shughuli za upandaji wa miti na uchakati wa mazao ya misitu katika viwanda vinavyozalisha mazao ya misitu vilivyopo wilayani Mufindi.

Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika kwa muda wa Siku mbili ikihushisha viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Viongozi kutoka Wilaya ya Mufindi, Wahifadhi kutoka Shamba la Miti Sao Hill pamoja na baadhi ya viongozi kutoka umoja wa wavunaji wa Shamba la Miti Saohill kuanzia Leo Jan 12 Januari 2025.