ACP Sisiwaya: Marufuku kuchanganya abiria na mizigo
17 September 2024, 10:40 am
Sheria za usalama barabarani zinakataza madereva wa magari ya abiria kupakia abiria pamoja na mizigo katika usafiri huo ili kuepukana na madhara endapo itatokea ajali.
Na Hafidh Ally
Wamiliki wa vyombo vya moto nchini wametakiwa kuhakikisha Madereva wa vyombo hivyo wanafuata Sheria za usalama barabarani na kuacha tabia ya kuchanganya abiria na mizigo wawapo safarini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa operesheni Kikosi cha Usalama barabarani nchini Tanzania Kamishna msaidizi wa polisi ACP Nassor Sisiwaya wilayani Mufindi mkoani Iringa kwenye operesheni maalum za ukaguzi zinazoendelea nchini kote na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia abiria kuwa salama.
ACP Sisiwaya amesema kuwa amewataka kikosi cha usalama barabarani kinaendelea na operesheni za kukagua magari yote na kupata stika ya Nenda kwa Usalama barabarani.
Naye Mkuu wa usalama barabarani mkoani Iringa, Mrakibu wa polisi SP Glory Mtui amesema kuwa, Jeshi la polisi limebaini kuwepo magari ya abiria yanayochanganya mizigo pamoja na abiria kitendo ambacho ikitokea changamoto ile mizigo inakuwa ya kwanza kuleta madhara kwa abiria.
Mtui amewakumbusha wananchi wote kuwa mabalozi wawapo safarini kwa kufichua utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya madereva kwa kuhatarisha usalama kwa watumiaji wengine wa barabara.
MWISHO