Wananchi Kiwele waomba josho la kuogeshea mifugo
26 April 2024, 9:58 am
Kuogesha mifugo ni muhimu sana kwani husaidia katika kudhibiti wadudu wanaosababisha magonjwa.
Na Joyce Buganda
Wananchi wa kata ya Kiwele iliyopo jimbo la Kalenga mkoani Iringa wanakumbana na changamoto ya ukosefu wa josho jambo linalopelekea kutembea umbali mrefu kwenda kuogesha mifugo yao.
Wakizungumza na kituo hiki baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa toka wameahidiwa kuwepo na josho la kuogesha mifugo yao imepita miaka mine huku wakienda katika kijiji cha Kiwele kufuata josho.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kijiji cha Mfyome Richard Luhala amesema kuwa kijiji cha Mfyome na Itagutwa vina idadi kubwa ya mifugo hivyo josho likiwepo katika vijiji hivyo itapunguza usafirishaji wa mifugo na kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Naye Diwani wa kata ya Kiwele Felix Waya amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na ameeleza kuwa endapo josho litapatikana kati ya kijiji cha itangutwa na mfyome itawapunguzia adha wafugaji ya kutembea kilomita 20 kupeleka mifugo kuogesha katika majosho jirani.