Bilioni 2.8 kufanya ukarabati wa chanzo cha maji bonde la Fukurwa
22 April 2024, 10:05 am
Uchakavu wa miundombinu ya maji katika chanzo cha maji bonde la Fukurwa chanzo cha upotevu wa huduma ya maji.
Na Mwandishi wetu
Jumla ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 2.8 zinahitajika ili kufanya ukarabati wa chanzo cha maji cha bonde la Fukurwa ili kukabiliana na upotevu wa maji ambao unasababishwa na uchakavu wa miundombinu ya chanzo hicho.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Makambako(MAKUWASA) Mhandisi Oscar Lufyagile wakati akizungumza kuhusiana na ripoti ya mgakuzi mkuu wa hesabu za serikali ambayo imezitaja mamlaka za maji za mkoa wa Njombe kuwa na upotevu wa maji kwa asilimia 39, ambapo amesema hali hiyo inachangiwa na uchakavu wa miundombinu ya maji ikiwemo bomba za kusafirishia maji pamoja na dira chakavu ambazo zimefungwa mwa muda mrefu kwa wateja.
Mhandisi Lufyagile amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hali ya upotevu wa maji katika mamlaka yake ilikuwa ni asilimia 31 na kueleza kuwa mahitaji ya maji kwa sasa ni lita milioni kumi na laki saba kwa siku na uzalishaji wa maji wa sasa ikiwa ni lita milioni 4.8 kwa siku sawa na asilimia 44 ya mahitaji yote.
Nao baadhi ya wananchi mjini Makambako, wameitaka serikali kuboresha miundombinu ya maji kwa kuondoa yote ambayo ni chakavu ili wananchi wapate huduma ya maji kwa wakati.
MWISHO