Viongozi wa Taasisi za serikalini Hatarini Kukosa Mishahara.
21 February 2024, 9:09 pm
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuzuia mishahara ya mwezi huu ya viongozi wa taasisi na idara za serikali, ambao mpaka sasa hawajaingia kwenye Mfumo wa Kielektoniki wa Usimamizi na Upimaji wa Utendaji Kazi Serikalini (PERMIS&PIMIS).
Pamoja na kuzuia mishahara hiyo, amelitaka Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma kuja na ushauri utakaowezesha kuwepo kwa uwiano wa mishahara ya watumishi wa umma tofauti na hali ilivyo hivisasa ambayo tofauti yake ni kubwa.
Amesema hayo leo wakati akifungua Baraza Kuu la Tano la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma linalofanyika mjini Iringa.
Akizungumzia mfumo huo pamoja na ule wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimali Watu (HR Assesment), Simbachawene amesema mifumo hiyo kama ilivyoelekezwa na serikali ni muhimu katika kupima utekelezaji wa majukumu ya mtumishi kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji wake, unaoendana na malengo yaliyowekwa kulingana na cheo, nafasi na taaluma yake katika kufikia lengo la taasisi na serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema moja ya majukumu ya Ofisi ya Rais -UTUMISHI ni kusimamia utumishi wa umma, na ndio maana serikali ikabuni mifumo hiyo inayotarajiwa kuboresha utendaji kazi serikalini kwa kumpima mtumishi mmoja mmoja na taasisi, huku kila waajiri katika ngazi mbalimbali wakiwa na uwezo wa kuona namna watumishi wao wanavyofanya kazi za kila siku.
“Tuliitana Dodoma, tukaelekezana, tukapeana na mbinu tujisajili kwenye mifumo ili data za kila mtumishi zikae vizuri, lakini inasikitisha baadhi ya watumishi, wengine wakiwa ni viongozi waajiri wa taasisi na idara za umma mpaka sasa hawajafanya hivyo,” amesema.
Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kusimamisha mishahara ya viongozi hao ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao na kuwapa muda watumishi wa kawaida, ili waweze kukamilisha utaratibu wa kuingia katika mifumo hiyo ambayo pia ni muhimu sana katika kupandisha madaraja na vyeo vya watumishi bila upendeleo.
“Mfumo huu kama tulivyojifunza uko wazi, unafanya upimaji wa utendaji kazi wa kila mtumishi bila upendeleo. Kwa hiyo utamlazimisha kila mtumishi kuwajibika huku mfumo ukimpima na kumfanyia tathmin, kazi ambayo awali ilifanywa kianalojia na kusababisha uzembe na malalamiko kati ya mpimaji na mpimwaji,” amesema Simbachawene.
Amesema kati ya watumishi wote wa umma nchini, watumishi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 31,000 bado hawajaingia katika mifumo hiyo, ambayo serikali ina matarajio makubwa kwamba itaimarisha utendaji wa utumishi wa umma kwa kutumia teknolojia.
Kuhusu uwiano wa mishahara, Simbachawene alisema; “Utumishi wa umma lazima uwe wa uwiano na kushabihiana kwa kipato. Tukiwa na watumishi wanaotofautiana sana kwa kipato inavunja moyo watumishi wengine. Lazima mambo kama haya ninyi kama baraza la wafanyakazi tushauriane ili kuondoa manung’uniko na chuki kwa serikali yao.”
Akitoa mfano Simbachawene alisema haiwezekani katika nchi moja kuwe na mtu mmoja ana mshahara wa Sh Milioni 30 huku sifa zake za kielimu, uzoefu na nyingine zinazohitajika katika utumishi zikiwa sawa au zinafanana na mtumishi anayelipwa chini ya Sh Milioni mbili.
“Hili jambo sio sawa kwa usalama wa nchi yoyote ile, tusipolishughulika mapema ipo siku litahama kutoka katika udhibiti wetu na kuleta shida kubwa. Ni lazima tuufanye utumishi wa umma kuwa utumishi mmoja wenye uwiano; tofauti ibaki kwenye tofauti ya kazi na maslai mengine lakini kwenye mishahara hata kama haipo sawa ni muhimu kuwe na uwiano,” alisema.
Awali Mwenyekiti wa baraza hilo, Juma Mkomi alisema kwa kupitia baraza hilo wajumbe wataelimishwa mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu na namna mifumo hiyo inavyofanya kazi, taratibu za uhamisho wa watumishi wa umma, na mambo muhimu ya kuzingatia kwa mtumishi anayejiandaa kustaafu.