Wananchi Mikumi wamshuru SSH kwa mradi wa Regrow
26 January 2024, 10:53 am
Na Mwandishi wetu.
Wakazi waishio pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Mikumi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanafanikiwa kubadilisha maisha yao kiuchumi kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Wanachi hao ambao wamejiunga kwenye vikundi vya Benki za Hifadhi za Jamii, (COCOBA) vilivyowezeshwa na Mradi wa REGROW wamebainisha hayo walipokuwa wakiongea na waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali waliofika kijijini hapo kujionea namna wananchi walivyonufaika na mradi huo.
Akitoa ushuda kwa timu ya wanahabari kwa kuwaonesha Nyumba anayojenga kupitia mradi wa REGROW, Bw. Hamisi Mayunga Tenela amesema kabla hajajiunga na COCOBA maisha yake yalikuwa ni magumu kutokana na kukosa kipato cha uhakika, lakini kupitia fedha za mkopo kutoka kikundi cha COCOBA, sasa anafanya biashara ya kukodisha baiskeli zaidi ya 50 na kuendesha Duka na Kutumia faida anayopata kujenga nyumba kubwa.
Akizungumzia mradi huo, Mwezeshaji Jamii wa REGROW Mikumi, Bi Neema Mgalambe, amesema, kupitia mradi huo, vikundi 15 vya COCOBA Mikumi vimeweza kutoa mikopo 623 yenye thamani ya shilingi 531,392,000 na marejesho ya mikopo hiyo ni shilingi 300,407,000.
Mradi wa REGROW unaotelekezwa kwa fedha za Mkopo kutoka Benki ya Dunia wenye masharti nafuu, unalengo la kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuboresha usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii nchini hususani Kusini mwa Tanzania.