Nuru FM

Wakurugenzi waaswa kutekeleza afua za mapambano dhidi ya Ukimwi

1 December 2023, 9:09 pm

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy akiwa anasikiliza taarifa kuhusu Afua za Mapambano dhidi ya Ukimwi. Picha na Adelphina Kutika

Na Adelphina Kutika

Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani Iringa pamoja na wadau wa maendeleo wanaoshughulikia masuala ya Ukimwi chini ya programu ya PEPFAR kuelekeza fedha kwenye shughuli za utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi.

Agizo hilo limetolewa  leo tarehe 01 Disemba 2023 katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika chuoni RUCU, na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema kuwa wakurugenzi watenge bajeti kwajili ya kuendeleza huduma za VVU na UKIMWI  katika halmashauri zao ili kuwa na huduma endelevu.

“Kama mkoa tunashuhudia kupungua kwa uwekezaji na Ufadhili  wawadau wa ndani na nje kwenye huduma ya VVU na UKIMWI naomba nitumie fursa hii kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kuweka kwenye bajeti na kuitengea fedha mipango na shughuli na kuendeleza huduma za VVU na UKIMWI ndani ya vituo na halmashauri zao.”Alisema Kessy

Kessy alisema jamii ya mkoa wa Iringa bado ina changamoto ya ushiriki  wa kutosha  kwenye kuongoza mwitikio kutokana na upungufu wa rasilimali fedha uwezo mdogo wa kiufundi  pamoja na mazingira magumu ya mwendelezo wa huduma za kinga na tiba dhidi ya VVU.

“Hii  pia inatokana na kuwa mkoa wetu ni wa pili kwa idadi ya maambukizi ya VVU ikianzia na mkoa wa Njombe ambapo una asilimia 11.4,Iringa 11.3  na Mbeya 9.3.’’Alisema kessy

Aidha alisema  katika kuelekea  95 ya kwanza  kuna changamoto  ya upimaji VVU  ikiwa unyanyapaa ,Ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU kwa baadhi ya maeneo,Ukosefu wa usiri kwa upande wa watoa huduma  wetu pamoja kutembea umbali mrefu kufuata huduma za dawa za kufubaza VVU.

Katika hatua nyingine Kessy aliwapongeza wakazi wa mkoa wa Iringa kwa kupambana na unyanyapaa hali iliyosaidia kuwapa fursa waathirika kutoka hadharani na kuendelea na shughuli za kimaendeleo.

“takwimu zilizofanyika  hivi karibuni zinaonyesha  kuwa mkoa wetu wa  Iringa unaongoza na kutokana na unyanyapaa ,mfano mkoa wa Kilimanjaro asilimia 19.5,Tanga asilimia10.5 na mkoa wetu wa iringa una asilimia 1.4 ndio mkoa pekee wenye asilimia ndogo ,hivyo niwaombe wananchi kumaliza kabisa asilimia hizo”Alisema kessy

Awali akiwasilisha risala Mbele ya Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Dr Christantus Ngongi Mratibu wa Huduma za Kudhibiti UKIMWI mkoa wa Iringa  alisema Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/2017 mkoa Iringa ni moja ya mikoa uliyonekana kuwa na maambukizi 11.3 huku wanawake wakiwa na maambukizi zaidi kwa asilimia 15.3 ikilinganishwa na wanaume asilimia 6.6.

‘’Mheshimiwa  kwa taarifa leo kwenye maadhimisho kama haya ngazi ya kitaifa tunatarajia kupata takwimu mpya za viwango vya ushamiri wa maambukizi ya VVU  ili kuona tunaelekea hatua gani katika kupambana dhidi ya maambukizi ya VVU”Alisema

Aidha mkoa kwa kushirikiana na wadau wanaotekeleza afua za mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi wameweka Malengo ya 95-95-95 yanalenga asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wale wanaojua hali zao wanapata matibabu ya kupunguza makali ya VVU na hatimaye asilimia 95 kati yao wanafikia kiwango cha chini cha VVU.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lekule aliwasihi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha Catholic RUCU   kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya  maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kutofanya ngono zembe.

“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha nyote tulioko hapana kwa namna ya pekee wanafunzi wetu kujiepusha na ngono zembe zinazoweza kupelekea maambukizi ya UKIMWI tujikinge wenyewe,tujilinde na tuwalinde wengine ” Alisema Prof.

Mstahiki meya wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada aliwata wakazi wa manispaa ya Iringa kuendelea kuchua taadhari juu ya   maambukizi ya VVU kwa kuwa mkoa wa Iringa bado upo katika nafasi ya pili kwa maambukizi UKIMWI.

Aidha maadhimisho hayo  yalikwenda sambamba na kauli mbiu “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI

Hata hivyo Madhumuni ya maadhimisho haya ni kutathmini hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI Kitaifa na Kimataifa na siku hii hutumika kuhamasisha na kuelimisha Jamii juu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, matumizi sahihi ya ARV kwa watu wanaoishi na VVU pamoja na kupinga unyanyapaa na ubaguzi.

Mwisho