Watumishi Mafinga Mji wapewa mafunzo ya mfumo wa kidijitali wa anuani za makazi
22 November 2023, 9:22 am
Na Hafidh Ally
Wananchi Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa wametakiwa kuacha tabia ya Kuharibu vibao vyenye majina ya Barabara na Mitaa ili visaidie kutoa maelekezo kwa wageni wanaotembelea Wilaya hiyo.
Kauli hiyo Imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt.Linda Salekwa alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Viongozi, Watendaji na Wataalamu kuhusu Utekelezaji wa matumizi ya Mfumo wa Kidigitali wa Anwani za Makazi Yaliyofanyika ukumbi wa Bomani Halmashauri ya Mji Mafinga na kuongeza kuwa Serikali haitasita kiwachukulia hatua wale wenye tabia ya kung’oa vibao hivyo.
Amesema baada ya Mafunzo haya Viongozi wanatakiwa kuwapatia Elimu wananchi wao kufahamu matumizi sahihi ya Anwani za Makazi na faida zake huku akiwataka Kuandaa Mpango kazi wa namna ya kushirikisha wananchi katika kutumia mpango huu wenye manufaa kwa Taifa na mtu mmoja mmoja.
Awali Mratibu wa Anwani za Makazi Kitaifa Mhandisi Jampyon mbugi amesema wameamua kuwajengea uwezo watumishi hao kutumia mifumo hiyo ili wawe mabalozi kwa wananchi wao kwani Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekuja na Mfumo wa Anwani za makazi ujulikanao kama NAPA unaosaidia kupata huduma zote za kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mh. Ayoub Kambi amesema kuwa Halmashauri yake imepanga kuhakikisha inatekeleza malengo ya Serikali kuufanya Mfumo wa anwani za Makazi Kidigital unatumika kwa wananchi wote.
Akizungumza kwa Niaba ya Regnant Kivinge ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri Mafinga Mji, Diwani wa Saohill Mh. Denis Kutemule amesema kuwa Kuna umuhimu mfumo huo utumike kwa njia za kawaida kwani unalazimu kutumia data na simu janja huku Baadhi ya maeneo ya vijijini yakikosa huduma ya Mtandao.
Nao Baadhi ya watendaji na watumishi waliopata mafunzo hayo wamesema kuwa watakuwa mabalozi Waziri wa mfumo huo kwani utasaidia kujua ni wapi huduma za kijamii kama Afya, hospital, Benki, Masoko na shule zilipo kwa kutumia mfumo huo bila kuuliza kwa Mtu.