Shilingi bilioni 70 zatengwa kuwalipa wakandarasi nchini
6 October 2023, 10:29 am
Na Frank Leonard
Serikali imetangaza kutenga Sh bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi wa ndani na nje wanaotekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Akitoa taarifa hiyo leo mara baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa Iringa, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 50 ni kwa ajili ya wakandarasi wa ndani.
Akizungumzia maendeleo ya uwanja huo, Bashungwa alisema utazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu na kuanza kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa Wananchi.
“Utakapoanza uwanja huu unatarajiwa kupokea ndege hadi za ukubwa wa Bombardier na utavutia watalii na kurahisisha huduma ya usafiri kwa maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta alitaja kazi zinazohusisha ukarabati wa uwanja huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege wenye urefu wa mita 2100 na upana wa mita 30.
Mengine ni maegesho ya ndege, barabara ya kiungio , taa za kuongozea ndege, uzio wa usalama, kituo cha zimamoto, ununuzi wa gari la zimamoto, kituo kidogo cha kufua umeme, jengo la muda la abiria na ununuzi na usimikaji wa mitambo ya kuongezea ndege.
Alisema hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 80 na akazitaja kazi zilizosalia na ambazo zinaendelea kutekelezwa kuwa ni pamoja na mfumo wa kuongezea ndege ambao umetekelezwa kwa asilimia 10.
Zingine ni ujenzi wa uzio uliotekelezwa kwa asilimia 30, jengo la zimamoto asilimia 90, jengo la nishati asilimia 90 na ununuzi wa gari la zimamoto linalotarajiwa kuwasili nchini kutoka Austria Desemba mwaka huu.
Alitaja moja ya changamoto ya mradi kuwani kuchelewa kwa malipo akisema mkandarasi wa uwanja huo kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd ya China anadai zaidi ya Sh Bilioni 14.8 pamoja na kwamba amelipwa zaidi ya Sh Bilioni 24.9.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa Salim Asas alisema kukamilika kwa barabara hiyo ya mchepuko kutapunguza msongamano, muda wa kusafiri, ajali na kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara za katikati ya mji.