Watumishi Sao Hill wapongezwa kwa utendaji
14 August 2023, 12:22 pm
Na Fabiola Bosco
Watumishi wa Shamba la Miti Sao Hill wilayani Mufindi mkoani Iringa wamepongezwa kwa utendakazi mzuri huku wakiaswa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo kwa maslahi ya umma na serikali .
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa shamba hilo la serikali huku akiwapongeza kutokana na uwajibikaji mzuri pamoja na kuwashughulikia wasiofanya kazi kwa uadilifu
“Kupitia taarifa ya mkuu wa hifadhi nawapongeza mnafanya vizuri ndo maana tunatamani wawekezaji waje wanunue miti kwetu na serikali ipate mapato lakini Hatutamvumilia mtumishi yeyote anayefanya kazi kwa mazoea” Mhe. Masanja amesisitiza.
Awali, alipokuwa akizungumza na wawekezaji katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu kwa nyakati tofauti, Mhe. Masanja aliwaomba wawekezaji wanaozalisha malighafi za misitu kuhakikisha wanatumia mazao ya misitu yaliyokomaa ili kuzalisha bidhaa bora.
Katika hatua nyingine Mh. Masanja alipongeza udhibiti wa moto kupitia taarifa iliyotolewa na muhifadhi mkuu wa shamba ambapo aliilionyesha matukio ya moto kupungua kulinganisha na miaka iliyopita
“Nawapongeza kwa kuweza kuhakikisha kuwa mmeweza kudhibiti utokeaji wa matukio ya moto kwa asilimia kubwa na kuhakikisha misitu yetu inalindwa, na pia mnatakiwa kuimarisha uhusiano mzuri na wananchi wanaolizunguka shamba ili kuepuka moto kutokea ovyo”.Amesema Mh. Mary Masanja
Ameendela kuitaka TFS kupitia watumishi wake kuendelea kuwapa elimu wananchi juu ya upandaji miti katika maeneo yao ili kusaidia uhifadhi wa misitu na kuboresha mazingira kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tuendelee kuhamasisha wananchi kupanda miti na kuwapa elimu ya umri gani ambao miti inatakiwa kuvunwa ili kuepusha kuwepo kwa bidhaa zitokazo viwandani ambazo hazikidhi viwango sokoni .”Amesema Mhe. Naibu Waziri
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mh.Linda Salekwa alimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufika na kutembelea Shamba la Miti SaoHill na wawekezaji wenye viwanda vinavyochakata mazao ya misitu waliopo ndani ya wilaya hii kwani kwa kufanya hivi kunawapa moyo na kuamini kuwa serikali ipo pamoja nao.
“Ujio wako unawapa faraja na kuzidi kuwapa matumaini kuona kwamba serikali ipo pamoja nao kwani wawekezaji hawa wanasaidia vijana wetu wengi katika wilaya kupata ajira viwandani humo”Amesema Dkt. Linda
Ziara ya Naibu Waziri Masanja Mkoani Iringa ni mwendelezo wa ziara zake za kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
MWISHO .