Mfuko wa sanaa kuwanufaisha wasanii Iringa
13 August 2023, 6:44 pm
Na Hafidh Ally
Mfuko wa utamaduni na sanaa Tanzania unatarajia kutoa Mikopo Mipya zaidi ya shilingi Bilion 20 kwa Wasanii hapa nchini katika mwaka huu wa fedha 2023/2024.
Hayo yamezungumzwa na Bi. Nyakaho Mturi Mahemba Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko wa utamaduni na sanaa Tanzania iliyopo chini ya Wizara Ya utamaduni Sanaa na Michezo katika semina ya kuwajengea uwezo wa namna ya kunufaika na fedha za mikopo wasanii mbalimbali Mkoani iringa iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Kleruu.
Bi Nyakaho amesema kuwa serikali ya awamu ya sita kupitia Mfuko wa sanaa imeamua kutatua changamoto ya wasanii ambayo ni Mtaji kwa kuwapatia fursa ya mikopo na elimu ya namna ya kuandaa sanaa zenye maslahi na kukuza uchumi wao.
“Tuna huduma tatu ambazo ni mikopo ya masharti nafuu, mafunzo na ruzuku na kuna Mikopo ya uendeshaji, mikopo ya vitendea kazi na Mikopo ya kujikimu na tunafanya kazi na benk ya NBC na CRDB na riba ya Mikopo hiyo ni Asilimia 9 ambayo inatozwa katika salio la mkopo” Alisema Bi Mahemba.
Amesema kuwa fedha hizo ni vyema zikelekezwa katika uzalishaji wa sanaa ambapo mpaka sasa wameshatoa zaidi ya Bilioni 1.07 kwa wasanii na kuna maombi ya milioni 17 huku wakiwa wanaendelea na mchakato wa kupitia miradi iliyoombewa fedha hizo.
Kwa upande Meneja wa Bidhaa na huduma kutoka Bank ya NBC Makao makuu Dar es salaam Jonathan Wilison Bitababaje amesema kuwa Benki yao imeingia katika kufanikisha zoezi la utoaji wa mikopo kwa watu wa sanaa na utamaduni ambapo mikopo hiyo ina masharti naafuu.
“Mikopo inayotolewa inaanzia kiasi cha shilingi laki 2 mpaka shilingi milioni 100 kwa mkopaji mmoja huku akiwataka wasanii kupitia ofisi za utamaduni Wilaya na Mkoa husika ili kujiandikisha na kuanza kunufaika na Mikopo hiyo” alisema Bitababaje
Mgeni Rasmi katika Semina hiyo Bi. Asifiwe Mwakibete Kaimu Katibu Tawala msaidizi Viwanda Biashara na uwekezaji amewataka wasanii hao kuhakikisha wanatumia fedha za mfuko huo vizuri katika kuinua sanaa na kazi zao kwa ujumla.
Amesema kuwa wasanii hao wametakiwa kuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo hiyo ili iweze kuwasaidia wasanii wengine waweze kunufaika huku akiwataka kuongeza ubunifu katika uzalishaji wa sanaa zao.
Naye Mwenyekiti Wa chama cha waigizaji Mkoa wa Iringa Hamis Nurdin ameishukuru serikali kwa kuwaletea fursa hiyo ya mikopo huku wakiahidi kuitumia vyema kwa kukopa fedha ambazo zitasaidia kuandaa sanaa ambazo zitakuwa na ubora.
Wasanii waliohudhuria semina hiyo ni wasanii wa muziki wa kizazi kipya, wasanii wa muziki wa asili, waigizaji wa filamu na tamthilia, vikundi vya ngoma za asili na washereheshaji (MC)