Polisi Iringa yakamata meno ya tembo, silaha
12 August 2023, 10:03 am
Na Frank Leonard
Oparesheni zinazoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, zimewezesha kukamata vipande saba vya meno ya tembo pamoja na silaha mbili zinazomilikiwa kinyume cha sheria.
Akizungumza leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema kwa kushirikiana na askari wa uhifadhi walimkamata Mathias Malenga (37) mkazi wa Image wilayani Kilolo, akiwa na silaha aina ya Shortgun isiyo na namba ikiwa na risasi mbili, gobore moja, goroli sita pamoja na mtego wa kuwindia wanyama.
“Halikadhalika Agosti 8, mwaka huu tulimkamata Jacob Mhanga (54) mkazi wa kijiji cha Utiga mkoani Njombe akiwa na vipande hivyo vya meno ya tembo katika nyumba ya kulala wageni katika kijiji cha Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa,” amesema.
Amesema katika oparesheni iliyofanyika kati ya Juni na Julai mwaka huu, jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watu tisa wakituhumiwa kuvunja na kuiba.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa na mali mbalimbali za wizi zikiwemo pikipiki nne, TV moja, laptop moja, jeki, spana, magodoro, cherehani mbili, baiskeli moja, mashine ya kutobolea na kuchomea na vitu vingine.
Katika kudhibiti magari yanayotembea usiku bila kufuata sheria za leseni za usafirishaji, alisema jeshi hilo lilikamata magari 12 yanayotembea usiku kwa makosa ya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ikiwemo kusafirisha abiria bila kufuata taratibu.