Ofisi za halmashauri wilaya Iringa zahamishiwa rasmi Ihemi
31 July 2023, 2:49 pm
Na Frank Leonard
Halmashauri ya wilaya ya Iringa imehamisha rasmi huduma zake za kiofisi katika majengo ya siasa ni kilimo mjini Iringa na kuzipeleka katika jengo lake jipya lililopo katika kijiji cha Ihemi, kilometa 35 kutoka mji huo, barabara kuu ya kuelekea Mbeya.
Jengo hilo la ghorofa moja limejengwa kwa Sh bilioni 2.7 ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati Dkt. John Magufuli lililozitaka halmashauri zote nchini kuwa na ofisi zake ndani ya maeneo yao ya utawala .
Uzinduzi wa utoaji huduma katika jengo hilo ulioanza leo umefanywa na mkuu wa wilaya ya Iringa, Veronica Kessy kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Iringa, Halima Dendego aliyewaagiza watumishi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanakuwepo siku zote za kazi na kutoa huduma kwa wananchi kwa viwango na ubora wa hali ya juu.
Mbali na vigezo vingi vilivyotumiwa na halmashauri hiyo kujenga ofisi hiyo kijijini hapo Kessy aliwashukuru wananchi wake kwa kukubali kutoa maeneo yao bila kudai fidia.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Steven Mhapa alikipongeza kijiji hicho akisema uamuzi wao wa kutoa eneo hilo umekiwezesha kupata jengo la kwanza la ghorofa katika historia yake.
Mhapa aliwataka watumishi zaidi ya 200 wa halmashauri hiyo kuhamishia uchumi wao katika kijiji hicho ili kuharakisha maendeleo yake.
“Msichelewe kutumia fursa zilizopo kijijini hapa. Jengeni nyumba za kuishi na za biashara zikiwemo nyumba za kulala wageni ili kwa muda mfupi kijiji hiki kipate hadhi ya mji mdogo,” alisema.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bashir Muhoja alitoa mchanganuo wa ujenzi wa ofisi hiyo akisema Sh Bilioni 2 zimetumika kukamilisha jengo hilo na Sh Milioni 700 zinajenga uzio utakaokamilika Oktoba mwaka huu.
Aidha alisema halmashauri hiyo inaendelea na ujenzi wa nyumba ya mkurugenzi inayojengwa kwa Sh Milioni 150 na nyumba tatu za wakuu wa idara zinazojengwa kwa Sh milioni 240.