Kanisa la EAGT Frelimo lakemea ukatili wa kijinsia, ushoga
27 July 2023, 11:12 am
Na Hafidh Ally
Kanisa ya EAGT Frelimo Manispaa ya Iringa limeweka mkakati wa kukemea matukio ya ukatili wa m kijinsia na ushoga kupitia ibada wanazoendesha.
Akizungumza na Nuru FM Mchungaji Ezekiel Yona Mwenda kutoka Kanisa la Evangelistics Assembless of God Frelimo amesema kuwa wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanakemea matukio hayo ambayo yamepelekea kuwepo na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Mchungaji Mwenda amesema kuwa wanashirikiana na dini zingine na madhehebu mengine kuhakikisha wanakemea matukio hayo ya ukatili na ushoga ambayo katika dini zote hayakubaliki.
“Sisi tuna utaratibu wa kukutana na viongozi wenzetu wa dini ya Kiislamu yaani mashekh na maustaadhi kwa ajili ya kuzungumzia masuala haya ambayo hayakubaliki katika vitabu vya Mwenyezi Mungu, na hata viongozi wa madhehebu mengine wamekuwa mstari wa mbele kukemea” Alisema Mchungaji Mwenda.
Mchungaji Mwenda ameyasema hayo kuelekea kilele cha wiki ya vijana wa kanisa la EAGT Frelimo ambapo watafanya shughuli za kijamii ikiwemo kuchangia damu, kufanya usafi na kushiriki bonanza ambalo kilele chake kitakuwa ni Julai 29 kwa kushiriki michezo kama kukimbiza kuku, kukimbia ndani ya magunia, kukimbiza bata na mchezo wa mpira wa miguu katika viwanja vya nyumba Tatu.
MWISHO