Mafinga Mji wakagua miradi ya maendeleo
21 July 2023, 10:10 am
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Michael Msite imefanya ziara ya kukagua Miradi mbalimbali ya Maendeleo Halmashauri ya Mji Mafinga.
Miradi iliyotembelewa ni Ujenzi wa Shule mpya ya msingi Muungano yenye Mkondo mmoja, Ujenzi wa machinjio ya kuku na Ujenzi wa vyoo soko jipya mtaa wa Pipeline Kata ya Wambi.
Akizungumza Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji Mafinga Dkt Aldonis Ulimboka amesema ujenzi wa machinjio ya kuku unatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani wenye thamani ya Tsh 38,327,600.00 Mradi huu utatoa huduma ya uchinjaji wa kuku ndani ya Halmashauri ya Mji Mafinga.
Lengo la Ujenzi wa machinjio ya kuku ni kuboresha usalama wa nyama, kuboresha afya ya mlaji , kuongeza ajira, kuboresha usafi wa nyama ili kudhibiti mgonjwa ya mlipuko na ujenzi umefikia 85 % ya ukamilishaji wake .
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwongozo Ndugu Cesilia Mbedule akitoa taarifa amesema ujenzi wa Shule mpya ya msingi Muungano unatekelezwa kupitia fedha za BOOST wenye thamani ya Tsh 347,500,000 ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu na wamefanikiwa kujenga jengo la utawala, vyumba viwili vya madarasa ya awali na matundu sita ya vyoo, vyumba saba vya madarasa ya elimu ya msingi, matundu kumi ya vyoo pia kichomea taka.
Faida za ujenzi wa shule mpya utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule mama ya mwongozo ujenzi umefikia 90% ya utekelezaji wake ambapo kazi ya ukamilishaji bado unaendelea.
Aidha akizungumza Afisa Biashara wa Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu Evance Mtikile kuhusu ujenzi wa vyoo soko jipya mtaa wa pipeline kata ya Wambi amesema mradi unatekelezwa na fedha kutoka mapato ya ndani ambapo ujenzi umefikia 10 % ya utekelezaji wake na kazi ya ukamilishaji unaendelea.
Ziara imehudhuriwa na wajumbe ambao Ni Waheshimiwa Madiwani wa Kamati hiyo,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Ndugu Charles Tuyi na Wataalamu.