Simba waliozua taharuki Iringa warudi hifadhini
6 July 2023, 11:29 am
Na Hafidh Ally
BAADHI ya Simba wala mifugo waliotokea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuzua taharuki kwa wananchi mkoani Iringa kwa zaidi ya siku 64 wanadaiwa kurudi hifadhini humo.
Akizungumza na kituo hiki Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki amesema Simba hao waliokadiriwa kuwa watano, waligawanyika katika makundi mawili, moja limerudi hifadhini na lingine lipo katika kijiji cha Isingo karibu na mashamba ya mwekezaji ambako kuna msitu mnene.
Akizungumzia idadi kubwa ya mifugo iliyouawa amesema hiyo ni kwasababu Simba hao walikuwa hawamalizi kumla mnyama mmoja na kushiba kwasababu ya taharuki na kelele walizokuwa wanakutana nazo kutoka kwa mifugo na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dedengo amewaondoa hofu wananchi hususani wa Iringa mjini akisema waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani Simba hao hawapo katika maeneo yao kama inavyotaarifa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo Taarifa za Simba hao ambao kwa mara ya kwanza zilitokea katika kijiji cha Magunga wilayani Iringa kabla ya kuelekea kijiji cha Kiponzero, Tanangozi na Sadani; wanadaiwa kuuwa mifugo 64 zikiwemo ng’ombe 34, mbuzi, nguruwe na kuku.
MWISHO