Bodi ya utalii TTB yaanza kampeni kutangaza utalii Nyanda za Juu Kusini
21 June 2023, 7:05 am
Mpanga Kipengele ni hifadhi iliyoko katika mkoa wa Njombe ikiwa ni miongoni mwa hifadhi zilizo chini ya mamlakaya hifadhi za wanyamapori Tanzania TAWA ina gharama nafuu ambazo kila mmoja anaweza kuzimudu.
Na Hafidh Ally
Bodi ya Utalii Tanzania TTB imeanza kampeni ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Nyanda za Juu Kusini kwa kumtumia balozi wa utalii nchini Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo mzee wa ‘fujo zisizoumiza’.
Akizungumza mara baada ya kufika katika hifadhi ya pori la akiba la Mpanga Kipengere lililopo mpakani mwa mikoa ya Njombe na Mbeya, Afisa Utalii Mwandamizi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania TTB Sany Tobiko amesema kuwa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wamepanga kuhakikisha malengo wanayafikia.
“Ziara ya Bongo Zozo imeandaliwa na bodi ya utalii Tanzania TTB chini ya mradi wa Regrow kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea vivutio vya Nyanda za Juu Kusini ambavyo ni Milima ya Udzungwa, Hifadhi ya Ruaha, Nyerere pamoja na pori la akiba Mpanga Kipengere. “Pia tutatembelea Kilwa kisiwani na Msongomnara katika ziara hiyo” alisema Tobiko.
Katika ziara hiyo wadau wa sekta binafsi za utalii kama kampuni za UPL Safari’s, Oxpecker Tour and Safari’s Co. Ltd, Bateleur Safari’s and Tours wamehamasika kuuza vifurushi vya watalii wa ndani na nje nchi na kushiriki na balozi wa utalii nchini Bongo Zozo ili kuhamasisha utalii katika kampeni hiyo.
Kwa upande wake balozi wa utalii nchini Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo mzee wa ‘Fujo Zisizoumiza’ amesema kuwa amefurahia ziara ya kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo kutembelea eneo la Mpanga Kipengere huku akifurahia zaidi kwenye maporomoko ya maji katika eneo hilo.
“Nimependa sana maporomoko ya maji ya Mpanga Kipengere, nimefurahia kuona pango alilojificha chifu Mkwawa wa Wahehe na katika eneo la kuteleza katika kivutio hicho na nitakuja na watoto wangu kwa ajili ya kuteleza, ninawasihi watanzania na watalii wa nje waje kufanya utalii katika pori la akiba la Mpanga Kipengere kujionea vivutio hivyo” Alisema Zozo
Kamishna mhifadhi msaidizi wa utalii Martha Philipo Msemo kutoka ofisi ya TAWA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini amesema kuwa pori la akiba Mpanga Kipengere lina mapomoko zaidi ya saba ambayo yana mvuto tofauti na lina ukubwa kilometa za mraba 1,574 ambapo wanafanya utalii wa kihistoria, utamadani na utalii wa mandhari.
Naye mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amewataka wananchi kufanya utalii wa ndani ili kukuza kipato na uchumi wa nchi huku akiwataka viongozi wa halmashauri kuweka sheria za kuhakikisha maporomoko ya maji yanatunzwa.
Hifadhi hiyo imeanza kupata watalii wa ndani na nje kufuatia uwepo wa vivutio mbalimbali maarufu ikiwemo pango linaloelezwa kwamba alijificha chifu wa Wahehe Mkwawa wakati wa vita, maporomoko ya maji zaidi ya saba na miamba ya aina mbalimbali.