Wafanyabiashara Iringa wagoma kufungua maduka
15 June 2023, 11:22 am
Na Mwandishi wetu
Wafanyabiashara mjini Iringa wamesitisha kutoa huduma za uuzaji wa bidhaa kwa kufunga maduka yote baada ya kuvunjwa kwa vibaraza vya nje ya maduka yao vinavyotumika kupanga bidhaa.
Zoezi hilo la uvunjwaji wa vibaraza hivyo limekuja baada ya kundi la wajasiriamali wadogowadogo almaarufu kama machinga kuondolewa eneo la Mashine Tatu lililopo katikati ya mji wa Iringa na kupelekwa eneo la Mlandege mjini hapo.
Uvunjwaji wa maduka pamoja na vibaraza umetajwa kufanyika nyakati za usiku, huku baadhi ya wafanyabiashara wakipata hasara kwa upotevu wa mali zao.
Akizungumzia tukio hilo Corla Bernito katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara JWT mkoa wa Iringa amesema kumekuwa na uendeshaji wa zoezi la kuvunja vibalaza “canopy” bila kushirikishwa na kuwa zoezi la Juni 14 mwaka huu mgambo na askari polisi wamevunja maduka na kuchukua bidhaa za wafanyabiashara.
Mkutano ulioitishwa alfajiri ya Juni 15 mwaka huu umesitishwa na polisi kwa madai kuwa hauna kibali.
Hata hivyo Halima Dendegu mkuu wa mkoa wa Iringa amewataka wafanyabiashara hao kusubiri katika mkutano huo ili azungumze nao, huku wafanyabiashara hao wakigomea kwenda katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo na kumtaka afike katika eneo la stendi kuu ya zamani ya mabasi walipokusanyika.