Jamii yatakiwa kufufua ndoto za wenye ulemavu Iringa
13 June 2023, 3:33 pm
Na Frank Leonard
Wadau wa mtoto mkoani Iringa wameilaumu jamii wakisema ndiyo inayotengeneza mazingira ya watoto wenye ulemavu kutojiweza na kukosa fursa za maisha yaliyo jumuishi.
Lawama hizo walizosema zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa ili kuleta suluhisho ya changamoto za maisha jumuishi kwa watoto hao zilitolewa kwenye mdahalo ulioandaliwa na Makutano TV na Rounding hands kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Iringa katika kuelekea kilele cha siku ya Mtoto wa Afrika.
Lengo la mdahalo huo lilikuwa ni kuchagiza malezi jumuishi na kukuza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa maisha jumuishi kwa watoto wenye ulemavu.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa amesema mazingira hayo ndiyo yanayosababisha watoto wenye ulemavu kukosa fursa wanazostahili na hivyo ndoto zao za kimaisha kupotea.
Katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata ujumuishi amesema mkoa wa Iringa umeendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolilenga kundi hilo ikiwemo utambuzi wa mapema, elimu, afya na uboreshaji wa miundombinu yao.
Akitoa takwimu za watoto wenye ulemavu Chuwa amesema mkoa wa Iringa una watoto 549 wanaoishi na ulemavu ukiwemo ulemavu wa viungo, kutokuona, ukiziwi, akili na albino.
Akitaja sababu za kuwaleta wadau wa mtoto kwa pamoja katika mdahalo huo, Jesica Mwalyoyo wa Rounding Hands alisema mbali na maisha jumuishi kwa watoto wenye ulemavu kutoridhisha lakini pia wamekuwa wakisahaulika katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
Nao baaadhi ya wadau waliopata nafasi ya kuchangia katika mdahalo huo kwa pamoja wameona ipo haja ya wataalam kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili watoto hao waweze kufikia ndoto zao kama watoto wengine wasio na ulemavu.
Aidha mmoja wa walemavu, Jema Mdegella ambaye kitaaluma ni mhasibu ametoa ushuhuda jinsi ilivyokuwa ngumu kwa jamii kumpokea hasa ilipofika wakati wa kwenda shule.
“Shule ilikuwa mbali, licha ya kuwa nina miguu yangu yote lakini kuna wakati ilinilazimu nitumie kiti mwendo ili kufika shuleni na kuna wakati ilinibidi kukaa chini kupisha watu wanaonishangaa kimo changu. Hakika imenichukua muda mrefu sana jamii kunikubali na kuishi na mimi,” amesema.
Zawadi Msigala mwanafunzi wa sheria wa Chuo Kikuu cha RUCU amesema ilimlazimu kulazimisha maisha jumuishi kwenye jamii yake pamoja na watoto wenzie kumkimbia kwa sababu ya ulemavu wake.
Mwongozo wa taifa wa utambuzi wa mapema na afya stahiki kwa mtoto mwenye ulemavu wa Septemba 2021 unaonesha ulemavu unaweza kuzuiliwa kwa asilimia 80 lakini pia utambuzi wa mapema wa ulemavu kwa mtoto unaweza kupunguza makali na athari za ulemavu ukubwani.