Wanahabari mkoani Iringa wahudhuria bunge la bajeti Dodoma kwa mwaliko wa mbunge Kabati
20 May 2023, 1:32 pm
Na Hafidh Ally
Waandishi wa habari mkoani Iringa wamehudhuria Bunge la 12, Mkutano wa 11 Kikao cha 29 cha Bunge la Bajeti kusikiliza Upitishwaji wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Wanahabari hao wamefika bungeni kwa mwaliko wa mbunge wa Viti Maalum mkoani hapa Dkt. Ritta Kabati ambapo mwenyekiti wa chama waandishi wa habari Mkoa wa Iringa Frank Leonard amemshukuru Mbunge huyo kwa kuwapatia fursa hiyo adhimu.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Malumu Mkoa wa iringa Mh. Ritta kabati amesema kuwa ameamua kuwapeleka waandishi hao bungeni kwa sababu wamekuwa na mchango mkubwa wa kuibua changamoto za wananchi wa iringa ambazo zinapelekea waweze kuwajibika.
Aidha Mh. Kabati amesema kuwa katika mwaka ujao atakapowakaribisha wanahabari Bungeni atawandalia banda ambalo litaizungumzia iringa katika muktadha wa lishe, ukatili na masuala ya ukimwi ili kuusadia mkoa huu.
WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kupitia Waziri Nape Nnauye ameomba kuidhinisha Sh bilioni 212.457.
Nape amesema Sh bilioni 30.503 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Sh bilioni 18.522 ni za mishahara na Sh bilioni 11.981 ni za matumizi mengineyo.
Aidha, Sh bilioni 181.953 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo Sh bilioni 146.777 ni fedha za ndani na Sh bilioni 35.176 ni fedha za nje.
MWISHO