Mbunge Kabati ahoji mpango wa serikali kukarabati barabara ya Nyang’oro
16 May 2023, 10:35 am
Na Hafidh Ally
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa iringa Dkt. Ritta Kabati ameiomba serikali kutenga fedha za kukarabati barabara ya Dodoma-Iringa katika mlima Nyang’oro.
Kabati ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu huku akihoji ni lini serikali itatenga fedha kwa ajili kuzuia mmomonyoko wa barabara hiyo ambayo imekuwa ikikuza uchumi wa Dodoma na Iringa.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mh. Atupele Mwakibete amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023 serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa miamba na udongo katika eneo la Nyang’oro ili kuja na mapendekezo ya kitaalamu ya kutatua changamoto hiyo.
Amesema kuwa wanaendelea na tathmini ya kumpata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo na mkataba utasainiwa kabla ya mwisho wa Juni 2023.
Katika hatua nyingine Mh. Atupele amempongeza Kabati kwa kufuatilia changamoto za barabara katika mkoa wa iringa huku akiahidi kuwa Wizara yake itaiweka barabara zi Mafinga na Kilolo katika bajeti ijayo ya serikali ili zitatuliwe kwa kiwango cha lami.