Baraza la Madiwani Mafinga laazimia kuwakamata wasiorejesha Mikopo ya Halmashauri.
29 April 2023, 12:14 pm
Madiwani wakiwa katika baraza la Madiwani. Picha Frank Leonard.
Na Frank Leonard
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Mafinga limeagiza kusakwa na kukamatwa kwa wanachama wa vikundi vilivyoshindwa kurejesha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu kati ya mwaka 2021 na 2022.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo inaonesha katika kipindi hicho vikundi hivyo (havikutajwa idadi) vilikopeshwa zaidi ya Sh Milioni 430 hata hivyo ni Sh Milioni 111 tu ndizo zilizorejeshwa.
“Zaidi ya Sh Milioni 320 hazijarejeshwa. Tunaomba wahusika wa vikundi hivyo wasakwe na wakikamatwa walazimishwe kutaja madiwani wanaotuhumiwa kushirikiana na vikundi hivyo kujipatia fedha kinyume na malengo yaliyotumika kuanzisha mikopo hiyo,” alisema diwani wa Kata ya Bumilahinga, Anderson Mwakyusa
Pamoja na marejesho hayo, Mwakyusa aliwaomba watendaji wa halmashauri hiyo kukifuatilia kikundi cha Mnyigumba ambacho peke yake kinadaiwa zaidi ya Sh Milioni 84.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Elias Msuya alisema wahusika wa vikundi hivyo watatafutwa na kuchukuliwa hatua, huku akitaja baadhi ya sababu inazozifanya baadhi ya vikundi vishindwe kufanya marejesho kuwa ni pamoja na miradi isiyo na uendelevu na kusambaratika.
Aidha baraza hilo limepokea taarifa ya mawakala wa pembejeo wanaotuhumiwa kufanya jaribio la udanganyifu katika biashara hiyo.
Bila kuwataja majina na udanganyifu huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira diwani wa kata ya Upendo, Michael Msite alisema April 16, mwaka huu mawakala hao ( hakutaja idadi yao) walisimamishwa kuendelea na biashara hiyo.
Hata hivyo alisema April 19, mwaka huu waliruhusiwa tena kuendelea kuuza pembejeo kwa wakulima kwa sharti la kuwasilisha barua ya utetezi kabla ya Mei 2, mwaka.
Msite alisema baada ya kuwasilisha barua zao za utetezi mawakala hao wanatakiwa kukutana na Waziri mwenye dhamana na kilimo pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Pembejeo (TFRA) kwa hatua zaidi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Regnard Kivinge amesema halmashauri yake imewafuta kazi watumishi wake watatu na wengine wawili wakisamehewa kwa sharti la kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa miaka mitatu.
Watumishi hao wamepewa adhabu hizo baada ya kukutwa na changamoto mbalimbali za kiutumishi ikiwa ni pamoja na utoro kazini na kutokuwa waaminifu.