Mbunge Sitta aibana serikali kuwapatia watumishi kada ya Elimu na Afya Jimbo la Urambo.
18 April 2023, 1:29 pm
Serikali imeombwa kuhakikisha inafikisha watumishi wa afya na elimu katika Jimbo la Urambo ili waweze kuwahudumia wananchi.
Na Hafidh Ally
Jimbo la Urambo Mkoani Tabora linakabiliwa na uhaba wa watumishi wa uma katika kada za afya na elimu jambo linalopelekea wamnanchi kuchelewa kupata huduma.
Hayo yamezungumzwa Bungeni Jijini Dodoma na Mbunge wa Jimbo la Urambo Mh. Magreth Sitta alipokuwa akichangia Hoja katika Wizara ya TAMISEMI na kuongeza kuwa Licha ya serikali kuwapatia madarasa, jimbo lake linakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi katika sekta ya elimu.
“Binafsi naipongeza serikali yetu Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia madarasa hivyo naomba katika zile ajira ambazo zimetangazwa basi na sisi tupatiwe Baadhi ili kuongeza idadi ya watumishi kwa wananchi wetu”, Alisema Sitta.
Mh. Magrerth Sitta amebainisha kuwa katika sekta ya elimu Jimbo lake linakabiliwa na uhaba wa walimu wa shule za msingi 639 na walimu wa sekondari 118.
Akizungumzia uhaba wa watumishi Katika sekta ya afya, Mh. Sitta amesema kuwa kuna upungufu wa wafanyakazi 758 huku akiiomba serikali kuwafikiria ikiwezekana na wao wapate watumishi katika ajira ambazo zimetangazwa na serikali hivi karibuni.
Wakati huohuo Mh. Sitta ameitaka serikali kutatua changamoto ya uhaba wa madawati kwa kuhakikisha mbao zinazokamatwa zinaelekezwa katika maeneo ambayo yana uhaba huo.