Watoto 172 Iringa Wanufaika Bima ya Afya
27 March 2023, 12:52 pm
Watoto 172 mkoani Iringa wamekabidhiwa bima za afya ili kuweza kumudu matibabu pindi wanapokabiliwa na magonjwa.
Na Adelphina Kutika.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Rounding Hands to Save Community na Makutano TV kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Iringa na Hidaya Catering mkoani Iringa wamekabidhi kadi za bima 172 kwa watoto wenye Mahitaji maalumu.
Akisoma taarifa ya Utekelezaji wa zoezi hilo Mkurugenzi wa Taasisi ya Rounding Hands to save Community Bi Jesca Mwalyoyo katika tukio la mtoto Bima lililofanyika katika viwanja vya kituo Cha Nyumba Ali ameeleza lengo la kutoa bima hizo ni kuwawezesha watoto kupata matibabu kwa wakati.
Akijibu taarifa hiyo Balozi wa watu wenye Ulemavu Tanzania na Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Iringa DK Ritha Kabati ameahidi kulipia bima za afya kwa watoto zipatazo 150 zilizosalia.
‘’Tujitahidi kutoa misaada mbalimbali kwa kushirikiana na wafadhili na watu wengine wenye mapenzi mema, lakini uhitaji ni mkubwa,hivyo tunawaomba watanzania na wadau wengine wajitokeze kuwasaidia watoto wenye ulemavu,’’alisema Ritha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa watu wenye ulemavu Shaaban Shomary na Zawadi Msigala wameiomba serikali kuhakikisha wanawasaidia upatikaji wa fursa nyingine Ili kutimiza malengo Yao na sio bima pekee .
Akitoa Shukurani kwa wadau waliofanikisha zoezi hilo Mkurugenzi wa Makutano Tv Tukuswiga Mwaisumbe amesema kipindi cha corona hali ya watoto ilikuwa hairidhishi ndio sababu iliyopelekea kuwawezesha bima hizo.
Hata hivyo wanufaika wa bima hizo ni watoto kutoka Shule ya Msingi Ipogolo kitengo maalum na Shule ya Msingi saba saba kitengo maalum ambapo tukio hilo limetanguliwa na maonyesho ya utoaji wa huduma ya elimu kwa watoto wenye ulemavu.
Uhitaji ni mkubwa,hivyo tunawaomba watanzania na wadau wengine wajitokeze kuwasaidia watoto wenye ulemavu.