Familia ya walemavu Kijiji cha Lulanzi waomba kupatiwa matibabu na chakula
14 March 2023, 8:26 pm
Na Hafidh Ally
Mama Mzazi wa Familia ya walemavu watatu wa familia moja anashindwa kumudu gharama za kuwalea watoto wake na kuwapatia matibabu.
Walemavu watatu wa familia moja katika Kijiji cha Lulanzi kilichopo Kata ya Mtitu Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa wamewaomba wadau wa maendeleo kuwasaidia kupata huduma ya matibabu na chakula.
Akizungumza na Nuru Fm, kwa niaba ya Ndugu zake, Catherine Mgogole akiwa na Mlezi wao Bi. Shilda Ignas Nyinge amesema kuwa licha ya kupatiwa Nyumba ya kisasa ambayo imejengwa kwa usaidizi wa fedha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia taasisi ya Isabella Foundation, bado kuna uhitaji wa kupatiwa chakula na matibabu ambayo yatakidhi mahitaji ya kila siku.
“sasa hivi tunashukuru tuna nyumba nzuri ila bado tuna uhitaji wa chakula pamoja madawa ili tuweze kutibiwa magonjwa yanayotusibu mara kwa mara” alisema Catherine Mmoja wa walemavu hao.
Kwa upande wake Balozi wa Utalii na uwekezaji Tanzania Bw. Harzy shija amesema kuwa alikutana na balozi mwenzake Isabella Mwampamba na kuona kuwa walemavu hao bado wana uhitaji wa chakula na dawa huku akiwaomba wadau wengine kuendelea kuwasaidia.
Naye Isabella Mwampamba Balozi wa Utalii Nchini ameahidi kuendelea kuisaidia familia hiyo kwa kushirikiana na wafanyakazi wake huko Jijini Arusha ili wapate vyakula.
“Mimi nimeshajiamua kuisaidia familia hii katika maisha yangu yote, hivyo nawaomba wadau wengine waweze kuwasaidia familia hii ipate chakula na fedha za matibabu” alisema isabella
Awali Diwani wa Kata ya Mtitu Mh. Rahman Mkakatu amesema kuwa kwa sasa familia hiyo iko katika mazingira bora baada ya kukabidhiwa nyumba ya kisasa ila kinachohitajika ni wanakijiji wa lulanzi na wadau wengine kujitoa kwa kuwapatia vyakula ili wajikimu kila siku.