Balozi Isabella atimiza ahadi ya kuwapeleka walemavu wa Lulanzi Hifadhi ya Ruaha
8 March 2023, 7:34 pm
Ziara ya kuwapeleka walemavu wa Kijiji cha Lulanzi katika hifadhi ya Taifa ya Rauha, ili kutalii na kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Na Hafidh Ally
Balozi wa Utalii Nchini Tanzania Bi. Isabella Mwampamba ametimiza ahadi ya kuwapeleka kufanya Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha walemavu watatu wa familia moja wa kijiji cha Lulanzi Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa.
Ahadi ya Balozi Isabella ilitolewa mwaka jana wakati Umoja wa wanawake watalii Nyanda za juu kusini ulipowatembelea walemavu hao kuwakabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinaadamu, huku Balozi Isabella akiahidi kuwapeleka kutembelea hifadhi hiyo kabla ya kuwabidhi Nyumba ambayo imejengwa kutokana na michango ya wadau wa Maendeleo na fedha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza wakati wa Ziara ya kuwapeleka katika hifadhi ya Taifa ya Rauha, Bi Isabella amesema kuwa familia hiyo ilipata wasaa mzuri wa kutalii na kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo.
“Ilikuwa siku bora sana kuwapeleka walemavu hawa katika hifadhi ya Ruaha, waliweza kufurahia na nawashukuru sana Hifadhi ya Ruaha kwa mapokezi mazuri waliyoyaonesha kwetu na huduma ambazo walizitoa kwa walemavu hawa” alisema Isabella
“Ilikuwa siku bora sana kuwapeleka walemavu hawa katika hifadhi ya Ruaha, waliweza kufurahia na nawashukuru sana Hifadhi ya Ruaha kwa mapokezi mazuri waliyoyaonesha kwetu na huduma ambazo walizitoa kwa walemavu hawa” alisema Isabella
Kwa upande wake Dada wa walemavu hao Faraja Lucas Mpogole amesema kuwa Ndugu zake wamefurahia sana kutembelea hifadhi hiyo huku wakionesha kufurahia zaidi kuwaona wanyama aina ya Twiga, Tembo, Nyati, Kiboko, Simba na ndege wenye Rangi nzuri za kuvutia.
Mama Mzazi wa Walemavu hao Angelista Kihanza amesema kuwa hakuwahi kufikiria kuwa ipo siku yeye na familia yake watapata fursa ya kwenda kutalii katika hifadhi yaTaifa ya Ruaha huku akimshukuru Isabella Mwampamba kwa kufanikisha ahadi hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na watoto wake.
Naye Afisa Muandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Bi. Amina Rashid Salum amempongeza Balozi wa Utalii Nchini Isabella Mwampamba kwa kuwapeleka walemavu hao katika hifadhi huku akikiri kuwa mwaka huu umekuwa wa bahati kwao baada ya kundi hilo kutalii.