Wanawake wenye Ulemavu Waiangukia Serikali
27 February 2023, 12:27 pm
Kutokana na changamoto wanazokumbana nazo watoto wenye ulemavu wawapo shuleni.
Na Fabiola Bosco.
Baadhi ya wazazi wenye watoto walio na ulemavu wameiomba serikali kuwakumbuka kwa kuwapa usaidizi wa namna ya kuwahudumia Watoto wenye ulemavu wawapo shuleni pamoja na upande wa mikopo ya asilimia kumi.
Wakizungumza na nuru fm wamesema wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali pindi wanapowapeleka watoto shuleni kutokana upungufu wa walimu wenye uzoefu wa kuwahudumia watoto wenye ulemavu.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa kata ya Isakalilo John Haruna amesema kuwa kila mtoto anahaki ya kupata elimu haijalishi ana upungufu gani hivyo ni vyema wazazi wenye watoto walio na ulemavu wakawasiliana na serikali za mitaa pindi fursa zinapotokea wakumbukwe zaidi.
Amesema kuwa utoaji wa taarifa unaweza pelekea wataalamu wakafika na kutambua ulemavu wa motto na kufahamu aina ya ulemavu alionao na shule anayopaswa kupelekwa kwa urahisi tofauti na kuwafungia ndani.
Kila mtoto ana haki ya kupata elimu na huduma za msingi kama binadamu wengine huku Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) ya mwaka 2000-2015 inaonesha watoto wenye ulemavu milioni 58 hawapo shuleni duniani na watoto milioni 100 hawamalizi shule.