Wanafunzi Wapewa Vyandarua
17 February 2023, 3:24 pm
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeunga juhudi za serikali ya awamu ya sita za kupambana na Malaria kwa kutoa vyandarua katika shule za msingi kwa kila mtoto.
Na Adeliphina Kutika.
Zaidi ya wanafunzi 230,000 wa shule za msingi 556 za Mkoa wa Iringa watanufaika na mpango wa serikali wa kugawa chandarua kimoja kwa kila mmoja wao kama sehemu ya mikakati ya serikali ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2030.
Mkakati huo ni mwendelezo wa juhudi za kitaifa na kimataifa kwa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazolenga kutokomeza Malaria katika nchi mbalimbali duniani.
Ugawaji wa vyandarua hivyo unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) umezinduliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Leonard Masanja katika shule ya msingi Ngome, mjini Iringa.
Meneja wa MSD Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini Robert Lugembe alisema kiasi cha Sh Milioni 400 kimetengwa kusambaza vyandarua zaidi ya 230,000 kwa shule hizo mkoani humo.
Wakati wa ugawaji wa vyandarua hivyo, Lugembe alisisitiza kuhusu usalama wake kwa matumizi ya binadamu akisema pamoja na viuatilifu vyake vimetengenezwa hapa hapa nchini.
“Hivyo kwa jamii kuvitumia kwa matumizi sahihi kutasaidia kuondoa kabisa maambukizi Malaria ifikapo 2030,” alisema Lugembe
Mpango wa kugawa vyandarua kwa wanafunzi hao umekuja huku Mkoa wa Iringa ukiwa umenufaika na programu kama hiyo mwaka 2020 iliyowezesha vyandarua 712,615 kugaiwa kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa.
“Hivyo kwa jamii kuvitumia kwa matumizi sahihi kutasaidia kuondoa kabisa maambukizi Malaria ifikapo 2030,” alisema Lugembe