Serikali Yatoa Milioni 50 Kumalizia Ujenzi Wa Zahanati Mtumile
16 December 2022, 5:13 pm
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeahidi kutoa fedha ili kumalizia ujenzi wa boma la zahanati ya Mtumile baada ya nguvu kazi za wananchi kufikia hatua ya kuezeka bati.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene katika Mkutano wa hadhara alioufanya katika kijiji cha Mtumile jimbo la Kibakwe Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa.
“Serikali itatoa shilingi millioni 50 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa boma la zahanati hiyo pamoja na kuanza ujenzi wa nyumba mbili za watumishi kwa kutumia fedha hizo.”
Nguvu zenu mlizojitolea na nguvu zangu nilizojitolea haziwezi kwenda bure, Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia kilio chetu.
Amefafanua katika mkutano wa Mkuu wa kumi wa Chama uliopita Mhe. Rais alielekeza viongozi kuhakikisha tunachapa kazi na kutenda haki kwa wananchi tunaowaongoza.
“niwaombe viongozi simamieni watu wafanye kazi, Kazi ya serikali ni kuweka huduma za msingi za kijamii ambazo zipo kwa kiasi kikubwa,” alisema waziri.
Akitoa salamu za kumkaribisha waziri, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Richad Maponda amesema kuna kazi nzuri zimefanywa katika jimbo la Kibakwe ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, elimu afya na umeme.
“tunapaswa kuungana na kiongozi wetu: kwa kumuamini katika kazi zilizotangulia kufanyika, maendeleo ni kupanga na kuchagua. huwezi kuyafanya yote kwa wakati mmoja, kuna mambo yatatangulia na mengine yatabaki.”
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtumile Bwn. Tito Mduwile ameishukuru serikali ya Awamu ya sita kwa fedha ilizopatia serikali ya kijiji ambazo zimesaidia kuimarisha miundo mbinu ya elimu na afya.
“kiasi cha Million 25 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa shule ya Msingi Mtumile, na kiasi kingine cha fedha za madawati zilizotolewa na wadau wa elimu ikiwa ni pamoja na fedha kutoka mfuko wa jimbo ambazo zimetumika kupauwa zahanati ya Mtumile.”