Nuru FM

Dc Moyo Athitibisha- Mama Na Binti Yake Kushikiliwa Na Jeshi La Polisi Kwa Tuhuma Za Kutoa Mimba

8 December 2022, 5:48 am

JESHI la polisi mkoani Iringa linamshikilia Mama mmoja anayejulikana kwa jina la Egria Ngalawa kwa tuhuma za kumtoa mimba binti yake mwenye umri wa miaka 17 na kufukia kichanga Kwenye banda la kufugia nguruwe lililopo nyuma ya nyumba yao katika mtaa wa Bomba mbili kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa.

 

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Iringa ambaye ni mkuu wa wilaya ya Iringa
Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa mtuhumiwa huyo anasadikika kutenda kosa hilo wiki moja iliyopita kwa mujibu wa taarifa alizopokea kutoka kwa raia wema.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Iringa ambaye ni mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiwa kwenye nyumba ya huyo mama kwa ajili ya kujiridhisha taarifa za tuhuma za kutoa mimba kwa binti wa mama huyo

Moyo alisema kuwa jeshi la polisi wilaya ya Iringa pia linamshikilia kwa mahojiano binti anayesadikiwa kutoa
mimba hiyo  na kushrikiana na mama yake kufukia kichanga hicho Kwenye banda la kufugia nguruwe.

 

Kiongozi huyo wa kamati ya ulinzi na usalama Iringa akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa kwa mujibu wa mahojiano Kati ya jeshi la polisi na watuhumiwa hao,inaelezwa kuwa mama wa binti huyo aliwahi kuitwa shuleni alipokuwa akisoma binti huyo nakutaalifiwa mwanae ni mjamzito.

 

Hata hivyo mama huyo aliyejulikana kwa jina la Agria Ngalawa amekana kuhusika kumtoa mimba binti yake na kufukia kichanga,akieleza kuwa Amekuwa akipokea malalamiko ya mara kwa mara ya binti yake kujihusisha kimapenzi na na wanaume za watu mtaani hapo.

 

Kwa upande wake binti huyo amekana kutoa mimba na kueleza kuwa hakuwahi kuwa na ujauzito wowote kwa kipindi hicho.

 

Aidha kulingana na maelezo hayo jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii limeanzisha
uchunguzi wa kisayansi ili kubaini kama binti huyo anakuwa na ujauzito za siku
za hivi karibuni na uchunguzi ukikamilika hatua za kisheria zitafuata.

 

Tukio hilo limeibuliwa katika siku kumi na sita za kupinga ukatilii ambapo mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ametumia jukwaa la maadhimisho hayo yaliyofanyika kiwilaya katika Kijiji cha Ikuvilo kukemea vitendo vya kikatili vinavyoendelea wilaya humo huku akiwataka wananchi kupaza sauti kuwafichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili hatua za kisheria zichuliwe dhidi yao.

 

Moyo aliwaoonya viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na kata kuacha tabia za kumaliza kiholela
kesi za ukatilii ikiwemo ubakaji na ulawiti huku akisisitiza yeyeto atakayebainika kufanya hivyo anafunguliwa mashtaka na serikali.