Iringa Yafanikiwa kuhamasisha wananchi wake kuwa na vyoo bora kwa asilimia 89.5
17 November 2022, 5:40 am
Mkoa wa iringa umefanikiwa kuhamasisha wananchi wake kuwa na vyoo bora kwa Asilimia 89.5 kati ya kaya 252,301.
Hayo yamezungumzwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa iringa Dr. Credianius Mgimba katika Maadhimisho ya Wiki ya usafi wa mazingira na Siku ya Choo duniani yiliyobebwa na Kauli mbiu isemayo “Kufanya yasioonekana kuonekana”
Dr. Mgimba amesema kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa iringa una jumla ya watu 1,197,728 ambapo kutokana na takwimu ya utekelezaji wa usafi wa mazingira kaya zenye vifaa vya kunawia mikono ni asilimia 77.
Alisema kuwa jumla ya Vijiji na Mitaa 189 sawa na asilimia 32.6 vimekabidhiwa vyeti vya ubora wa vyoo na usafi wa mazingira hadi mwaka 2021 ambapo kuna vijiji 148 ambavyo vimekidhi viwango vya ubora na usafi na vimekadhiwa vyeti katika maadhimisho hayo.
“Kutokana na kauli mbiu yetu hii ya Kufanya yanayoonekana kuonekana tunataka kuhamasisha wananchi wazingatie usafi kwani watoto zaidi ya mia 8 hufariki kutokana na kutokana na kuharisha kunakohusishwa na kutumia maji ambayo siyo safi na salama na usafi duni wa mazingira ikiwemo kueneza usafi wa kinyesi cha binaadamu katika vyanzo vya maji’ alisema Mgimba
Alisema kuwa kuna kuchangamoto hafifu ya udhibiti wa uchaguzi wa maji yaliyokuwa ardhini pamoja na ujenzi holela wa makazi ambao hauzingatii mabadiliko ya teknolojia kwani vyoo vingi hubomoka na kuririsha maji katika makazi ya watu na kuleta madhara katika jamii.
Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Kimataifa UNICEF Mkoa wa Iringa Remigius Sungu amesema kuwa shirika lao litahakikisha linashirikiana na serikali Mkoani hapa kwa rasilimali fedha na wataalamu ili kuhakikisha wanaboresha mazingira ya usafi wa vyoo na mazingira kwa ujumla.
Amesema kuwa shirika lao limekuwa likihamasisha shughuli za usafi wa mazingira kupitia Klabu za usafi wa mazingira katika shule za msingi ili kuwafanya watoto kuwa katika mazingira bora ya kujifunza.
Naye Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo ya wiki ya usafi wa mazingira na siku ya choo Duniani Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mh. Peresi Magiri ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote Mkoani hapa kuhamasisha wananchi wao kuwa na vyoo bora ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko yanayosababisha vifo.
Amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha wananchi wanajenga na kutumia kwa usahihi vyoo bora ili kudhibiti uchafuzi wa maji ardhini ifikapo mwaka 2030.
“tuna lengo ifikapo mwaka 2030 tuweze kudhibiti uchafuzi wa maji ardhini na ili kutekeleza azima hiyo ni lazima tuanze sasa kwa kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora ambacho kina viwango” alisema Peresi.
Maadhimisho ya Wiki ya usafi wa mazingira na Siku ya Choo duniani kimkoa yamefanyika katika halmashauri ya Wilaya ya Iringa huku Mkoa wa Iringa ukionekana kuwa na kaya zenye vyoo bora.