Nuru FM

Mbunge Kabati Ahoji mkakati wa Kuhamasisha wanawake kuchimba madini- Agusia Nyakavangala

2 November 2022, 5:25 pm

Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Iringa Kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Dr Ritta Kabati ameihoji serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha wanawake kujihusisha katika sekta ya uchimbaji wa madini.

Mbunge Kabati ametoa hoja hiyo bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 wanawake wameonekana ni wengi zaidi hivyo wana ulazima wa kujihusisha katika uchimbaji wa madini ili kujipatia kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati akiwasilisha Maswali yake Bungeni Jijini Dodoma katika Wizara ya Madini

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati akiwasilisha Maswali yake Bungeni Jijini Dodoma katika Wizara ya Madini

Katika swali la Pili Mbunge Kabati alitaka kujua ni hatua gani ambazo zinafuata baada ya utafiti wa awali kuonesha kuna madini ya dhahabu katika eneo la Nyakavangala ili kukuza uchumi wa Mkoa wa iringa.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali imefanya utafiti wa awali kubaini uwepo madini ya dhahabu katika eneo la Nyakavangala Lililopo Mkoani iringa ili kutambua mikondo yenye dhahabu na kuanza kuyachimba.

Aidha Dkt. Kiruswa amesema kuwa miongoni mwa madini yanayopatika na katika eneo la Iringa ni Dhahabu katika maeneo ya sadani ikweha malenga makali ilolo ifunda kalenga idodi na pawaga, Shaba katika maeneo ya mahenge kiwele pawaga, nyang’oro, malenga makali,  madini viwanda aina ya chokaa yanapatikana ifunda kiwele idodi na kuhongota.

Katika hatua nyingine Naibu waziri Kiruswa amesema kuwa mpaka sasa wanawake wameaanza kunufaika na sekta ya madini kwani mpaka sasa wametoa leseni 20 katika vikundi vya wanawake wanaojihusisha na uchimbaji wa madini.

Amesema kuwa wizara ya madini imemteua Mbunge Ritta kabati kuwa Miongoni Mwa Mabalozi Wa Madini hapa nchini ambao wameonesha kuwa vinara wa kuhakikisha wanawake wanafaidika kupitia sekta ya madini.

MWISHO