Viongozi Manispaa Ya Iringa Watakiwa Kuzingatia Maslahi Ya Watumishi
28 October 2022, 8:39 am
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameutaka uongozi wa Manispaa ya Iringa kuzingatia mahitaji na maslahi ya watumishi ili kuwajengea ari na morali ya utendaji kazi katika kuwahudumia wananchi.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa viongozi wa Manispaa ya Iringa, wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa hiyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamozo zinazowakabili watumishi hao.
Mimi naomba sana viongozi mbadilike katika suala zima la kusimamia rasilimaliwatu, tuzingatie maslahi na mahitaji ya watumishi wetu ili kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii, weledi na morali ya hali ya juu, Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka wakuu wa idara katika Manispaa ya Iringa kuwa na utaratibu wa vikao vya mara kwa mara na watumishi wanaowasimamia ili kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati.
“Si jukumu la Mkurugenzi au Afisa Utumishi pekee kuzungumza na watumishi, wakuu wa idara mnawajibu wa kuwa na vikao vya kuzisikiliza kero na changamoto zinazowakabili watumishi mnaowaongoza ili kuzitatua, Mhe. Ndejembi amehimiza.
Kuhusiana na wingi wa malalamiko kutoka kwa watumishi, Mhe. Ndejembi amesema, uongozi wa Manispaa ya Iringa unapaswa kufanya tathmini ya hali ya utendaji kazi kwani idadi kubwa ya watumishi imewasilisha malalamiko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Mohammed Moyo amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutenga muda wa kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi katika wilaya yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi Mkoani Iringa iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.