Waziri Mkenda Ataka Chuo Cha DIT Kuongeza Mafunzo Kwenye Ujuzi Wa Bidhaa Za Ngozi
8 October 2022, 7:39 am
Serikali imeitaka Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Saalam (DIT) kuhakikisha kuwa inaongeza ufundishaji kwenye ujuzi wa bidhaa za ngozi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo wakati alipotembelea chuo hicho kampasi ya Mwanza ili kujionea maendeleo ya taasisi hiyo ikiwemo mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Teknolojia ya Ngozi unaoendelea chini ya Kampuni ya Comfix Engineering.
Amesema kuwa Serikali imetenga Shillingi Bilioni 19.6 kwa ajili ya ukarabati wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Saalam (DIT) Kampasi ya Mwanza utakaoleta mapinduzi ya elimu kwa vitendo katika teknolojia ya ngozi nchini.
Prof. Mkenda amesema serikali inafanya ukarabati huo katika mpango wake wa kuhakikisha DIT inakuwa kitovu cha utoaji mafunzo ya ufundi wa utekengenezaji bidhaa za ngozi ikiwa ni pamoja na viatu, mikanda, waleti, mabegi na mipira jambo ambalo litasaidia kutengeneza ajira kwa vijana wengi kanda wa ziwa na Tanzania kwa ujumula.
“Kupitia DIT vijana wengi wanaweza kupata ajira, tunahitaji tuwe na vijana wenye ujuzi kutoka kwenye chuo hiki wanaoweza kujiajiri na kuwa chanjo cha ajira kwa wengine,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akitoa taarifa kwa Waziri huyo ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ya DIT ambayo ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya teknolojia ya viwanda vya ngozi nchini.
Awali Mwenyekiti wa baraza la DIT Mhandisi Dkt. Richard Masika akimkaribisha waziri wa elimu katika taasisi hiyo amesema DIT imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi wa utengenezaji bidhaa za ngozi kwa nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo vijana wa waweze kushindana katika soko la ajira kitaifa na kimatafa.
“Kwa sasa tunafundisha wanafunzi wetu utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa kutumia mashine na mikono ili hata wakitoka hapa waweze kutejitengenezea ajira wao wenyewe,” amesema Dkt. Masika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ameanza ziara ya siku nane katika mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ni mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita na Kagera.