Bungeni: Wenye malimbikizo ya madeni ‘walegezewa kamba na TRA’
17 September 2022, 7:21 am
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inaendelea kujadiliana na wafanyabiashara wenye malimbikizo ya kodi, ili kuwapa unafuu wa malipo kwa awamu bila kuathiri mwenendo na uendeshaji wa biashara zao.
Chande ameyasema hayo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma kuhusu hatua zinazochukuliwa kwa walipa kodi walioshindwa kulipa na kuwa na malimbikizo makubwa lakini wapo tayari kulipa kutokana na agizo la Rais.
Amesema, “Sheria ya Usimamizi wa Mapato, Sura 438 Kifungu cha 70 na Kanuni zake kinampa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusamehe adhabu na riba kama kuna suala na sababu maalum na majadiliano yanayoendelea ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.”
Awali, Naibu Waziri Chande alisema Serikali ilifuta utaratibu kulipa kodi kabla ya kuanza biashara, ili kutoa nafasi kwa Wafanyabiashara kujiimarisha ikiwa ni jibu la Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Athuman Katimba, aliyetaka kujua Serikali itaondoa lini utaratibu wa kulipia kodi biashara mpya kabla ya kuanza biashara husika.
Amesema, baada ya Serikali kufuta utaratibu huo mwaka 2019/20, wafanyabiashara wanatakiwa kulipa kodi miezi sita baada ya kufungua biashara, na kusema utozaji wa kodi ya mapato huendana na mapato yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka husika huku akiiagiza TRA kutekeleza sheria, ji wake wa kazi.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linaendelea na vikao vyake vilivyoanza Septemba 13, 2022 ambapo maswali na majibu kwa Wizara mbalimbali yamekuwa yakiendelea kutolewa na kujibiwa, huku hoja mbalimbali zikipatiwa ufumbuzi na maelekezo kutoka kwa kiti cha Spika.