Karani Wa Sensa Aona Miti Badala Ya Nyumba-Tabora
6 September 2022, 10:16 am
Mratibu wa wa sensa katika Wilaya ya Igunga Ally Hemed amesema kwamba Karani wa Sensa wilayani Igunga mkoani Tabora, alishindwa kuifikia kaya moja iliyopo katika kijiji cha Migelele, Kata ya Lugubu wilayani humo baada ya kuchezewa kiini macho na kuona miti kila alipoisogelea nyumba hiyo..
Katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 katika Mkoa wa Tabora ambacho kimefanyika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi kikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora balozi Dkt .Batilda Burian ambacho pamoja na mambo mengine kililenga kupokea changamoto ambazo ziliibuka katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Akiwasilisha sehemu ya changamoto Mratibu wa wa sensa katika Wilaya ya Igunga Ally Hemed alisema kulitokea kaya moja katika kijiji cha Migelele kata ya Lugubu ambayo karani alikuwa akiona miti kila alipoisogelea kwa ajili ya kwenda kutekeleza jukumu lake hali iliyo kwamisha zoezi hilo katika siku ya kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo alisema kwamba changamoto hiyo ilitatuliwa baada ya kuwahusisha wazee wa Kijiji hicho na hatimaye kufanikisha zoezi la kuhesabu kaya hiyo ambayo ilikuwa na mtazamo wa kutokuhesabiwa.
“Tulifanikiwa kuendelea na zoezi la sensa baada ya kuwashirikisha baadhi ya wazee wa kijiji hicho ambao walitoa ushirikiano kwa kamati ya sensa ya wilaya na kata kwa ajili ya kufanikisha na kuondoa changamoto hiyo’’ alisema mkuu wa wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo
Awali akifungua kikao hicho cha tathimini ya utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 mkuu wa mkoa wa Tabora wa Tabora balozi Dkt .Batilda Burian alisema kwamba katika zoezi hilo wananchi wa mkoa wa Tabora ndio waliopelekea kufaniksha kwa zoezi la Sensa ya mwaka 2022 kwa zaidi ya Asilimia 100 .
Alisema kwamba sensa ni tukio linalofanyika mara moja tu kila baada ya miaka kumi lakini takwimu zitokanazo na Sensa zitatumika kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.
“Sote tunafahamu kwamba, zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi muhimu Kitaifa, Kikanda na Kimataifa “alisema balozi Dkt .Batilda
Mkuu huyo wa mkoa wa Tabora alisema kwamba zoezi hilo litatuwezesha kutupatia takwimu muhimu zitakazosaidia kupanga, kupima na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kisekta na mipango ya maendeleo ya umoja wa Mataifa ambayo Tanzania imeridhia na inatekeleza.