Ujenzi wa Nyumba ya walemavu Lulanzi Wilaya ya Kilolo wafikia asilimia 80 kukamilika
26 July 2022, 4:18 pm
Zoezi la ujenzi wa nyumba ya Familia ya watu watatu wenye ulemavu katika kijiji cha lulanzi Kilichopo Kata ya Mtitu Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa Limefikia asilimia 80 ili kukamilika.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Chuo Cha RDO Kilolo Mwl. Lustice Ndokole ambacho kimepewa Kandarasi ya ujenzi wa Nyumba hiyo na kuongeza kuwa kazi iliyobaki ni kupaka rangi, kuweka mfumo wa umeme, mfumo wa maji pamoja kufunga Dari.
Mwl. Ndokole amesema kuwa Chuo cha RDO Kilolo kimetumia muda mfupi mpaka kufikia hatua hiyo ya ujenzi wa Nyumba hiyo huku akimpongeza Balozi wa Utalii Isabella Mwampamba kwa kuwafikishia vifaa vya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo vikiwemo vifaa vya Umeme,mabomba ya maji na Masinki ya Chooni.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Nyumba Hiyo, Diwani wa Kata ya Mtitu Mh. Rahman Mkakatu amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Nyumba Hiyo inayojengwa kwa usimamizi wa Taasisi ya Isabella African Foundation iliyo chini ya Balozi wa Utalii Nchini Tanzania Isabella Mwampamba.
Aidha Mh. Mkakatu amemshukuru Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Wadau wa Maendeleo na wananchi wa Kijiji Cha lulanzi ambao wameshiriki kuhakikisha mradi wa ujenzi wa nyumba hiyo unakamilika huku akiwataka wadau wengine kuendelea kuchangia mahitaji ya ujenzi wa nyumba hiyo kupitia namba ya 0762-756046.
Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Lulanzi Luka Idd Kihongosi amesema kuwa ujenzi wa Nyumba hiyo utasaidia familia hiyo kuishi katika mazingira mazuri ambayo hapo awali walikuwa wakiishi katika mazingira yasiyoridhisha.
Naye Mama Mazazi wa walemavu hao Anjelista Kihanza akiwa na watoto wake amesema kuwa wanafurahia zoezi la ujenzi wa nyumba hiyo ambayo inatarajia kukamilika hivi karibuni huku wakiwaombea dua Balozi Isabella Mwampamba kwa kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Balozi wa Utalii Nchini Bi.Isabella Mwampamba ambaye ndiye Mratibu wa Ujenzi wa Mradi huo amesema kuwa anatarajia kufanya uzinduzi wa nyumba hiyo wiki ya Mwisho ya mwezi wa nane ambapo uzinduzi wake utaenda sambamba na kuwapeleka Walemavu hao kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa siku Mbili.
Aidha Balozi Isabella amewashukuru Wadau wote walioshiriki katika zoezi hilo wakiwemo Bodi ya utalii, Wafanyakazi wa TANAPA, ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Kilolo, Watumishi Wilaya ya Kilolo, Watumishi wa ALAF Arusha, baadhi ya wafanyakazi wa matawi ya Benki ya CRDB Dodoma, Kampuni ya Mabasi Machame,Taasisi Bulk, Wazazi na wafanyakazi wa upendo friends school.
MWISHO