TBS Yateketeza Bidhaa Za Vyakula Na Vipodozi Katavi
11 June 2022, 8:17 am
BIDHAA mbalimbali za vyakula na vipodozi vyenye thamani takribani ya shilingi za Kitanzania milioni 7 zimeteketezwa katika dampo la Manispaa ya Mpanda baada ya kukutwa hazikidhi viwango kwa mujibu sheria ya Viwango Na 2 Sura 130.
Bidhaa hizo zilizoteketezwa mjini Mpanda ( 10/06/2022 )zilikamatwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi kwa ushirikiano na ofisi ya Kamanda Polisi, Katibu Tawala, Mamlaka ya Mapato na uongozi wa wilaya katika operesheni iliyofanyika Februari, Aprili na Mei, mwaka huu Mkoa wa Katavi katika Halmashauri zote za mkoa huo ambazo ni Manispaa ya Mpanda, Mlele, Mpimbwe, Tanganyika na Nsimbo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteketezwa kwa bidhaa hizo Kaimu Meneja TBS Kanda ya Magharibi, Rodney Alananga, alisema bidhaa hizo zilikamatwa maeneo ya mjini na vijijini katika maghala, maduka ya rejareja, jumla, supermarkets, masoko ya mipakani na stoo.
“Kati ya maeneo zaidi 100 yaliyokaguliwa, 36 yalikutwa na makosa kuuza au kuhifadhi bidhaa zilizokwisha muda, zenye viambata sumu, zisizosajiliwa na nyingi zinaingia nchini kwa njia zisizorasmi na mengine kukosa vibali vya kuuza au kusambaza vyakula na vipodozi toka TBS hivyo kuweza kuhatarisha afya na uchumi wa nchi,” alisema Alananga
Kwa mujibu wa Alananga, vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku zaidi ya aina 20 vilikamatwa ni pamoja na carolight, top lemon, clair men, diproson, Citrolight,carotene,Extra clair,clinic clear, betasol,prince clair, tent Claire, G&G na vingine.
Alifafanua kwamba bidhaa hizo zikitumiwa zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa kusababisha magonjwa ya ngozi na Kansa:mfano kutoka mabaka au vipele sehemu mbalimbali za mwili na pia kuleta madhara ya mfumo wa uzazi au mzio wa ubongo wa watoto kwa mama wajawazito.
“Vilevile vinaweza vikachangia kuleta Kansa ya ngozi na damu na hata kifo,” alisema na Alananga na kuongeza;
“Vilevile vyakula vilivyokamatwa ni vile vilivyokwisha muda wake wa matumizi ambavyo si chakula salama kutumiwa ambapo ilibidi kabla ya ukaguzi wa serikali wamiliki wanalazimika kujikagua, kutoa taarifa na kukabidhi hizo bidhaa kwa ofisi ya Afya na mazingira ya Halmashauri kwa ajili ya kuteketezwa kwa taratibu zilizopo.”
Alitaja bidhaa hizo kuwa ni kama vinywaji mbalimbali, sabuni, biscuits, Blue bands, hamira, viungo mbalimbali.
“Havifai kwa matumizi sababu vinaweza leta madhara mbalimbali ya kiafya kama kuumwa tumbo na hata kansa,” alisema.
Alisema hatua zilizochukuliwa wakati wa operesheni ni kutaifisha bidhaa, kulipishwa tozo za uteketezaji ikiwemo gharama zote za usafirishaji, dampo na miundombinu na usimamizi wa uteketezaji.
Alananga alitoa wito kwa wafanyabiashara kuzingatia sheria na kutumia vizuri na kwa vitendo elimu na mafunzo wanayopata mara kwa mara kutoka TBS na wataalam wa mkoa na Halmashauri ili kushirikiana na serikali awamu ya sita katika kulinda afya za Watanzania na kukuza biashara kwa kuuza au kuingiza bidhaa bora na salama katika soko la Katavi.
Alisema ni muhimu wananchi kujenga tabia ya kusoma maelezo ya lebo katika bidhaa, kununua bidhaa za vyakula na vipodozi katika maduka yaliyotambuliwa na TBS, kudai risiti za manunuzi na kutembelea tovuti ya shirika kujua vipodozi na vyakula vilivyosajiliwa na kuthibitishwa.
Aidha, aliwataka wananchi na wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa TBS na vyombo vya dola hasa kutoa taarifa pale ambapo wanaona kuna wafanyabiashara wanakiuka taratibu hizi.