Ujenzi Wa Nyumba ya Walemavu Lulanzi Wilaya ya Kilolo Waanza
12 May 2022, 7:53 am
Hatimaye familia ya watu watatu wenye ulemavu iliyopo kijiji cha Lulanzi Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa imeanza kujengewa nyumba ya kisasa.
Akizungumza mara baada ya kuanza kwa ujenzi huo katika hatua ya msingi, Balozi wa Utalii Nchini Isabella Mwampamba ambaye anasimamia zoezi hilo chini ya Taasisi yake ya Isabella African Foundation, amesema kuwa wameamua kujenga nyumba ya kisasa ambayo itakuwa na huduma zote muhimu ndani yake.
Amesema kuwa mafundi wameshachimba msingi wa nyumba hiyo ambayo itakuwa na vyumba viwili vya kulala na choo ndani huku nyumba ya sasa ambayo walemavu hao wanaishi ikitarajiwa kuwa jiko pamoja stoo ambapo mradi huo ukitarajiwa kukabidhiwa tarehe 31/7/2022 mara baada ya kukamilika.
Bi. Isabella amebainisha kuwa hapo awali akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo na Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mh. Justine Nyamoga walikubaliana kuwajengea Jiko, lakini alivyofika katika familia hiyo tarehe 4/5/2022 aliwaona walemavu hao wakipata shida kwenda chooni hivyo akaona ni bora kuwajengea nyumba yenye choo ndani huku nyumba wanayoitumia kwa sasa ikitarajiwa kuwa jiko na stoo.
Amesema kuwa hatua hiyo ni mafanikio ya harambee ya kuwachangia walemavu hao iliyofanyika tarehe 5/5/2022 katika Ofisi ya kwa mkuu wa wilaya ya kilolo yenye lengo kutafuta shilingi milioni 20 ambapo hata hivyo ilipatikana shilingi milioni 10 huku Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa akitoa shilingi Milioni 5 ambazo tayari zimeshawekwa kwenye akaunti ya Wadau wa maendeleo ya Wilaya ya Kilolo.
Awali Liliani Mbedule maarufu kwa Jina Lili Toto Shop ambaye ni Mfanyabiashara Mkoani iringa aliwasihi wananchi na wadau wa maendeleo kuwa na moyo wa kuwasaidia watu wenye ulemavu kutokana na changamoto ambazo wanazipitia.
Naye Dada wa walemavu hao Pelaja Mpogole amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kuwachangia shilingi Milioni 5 huku akimshukru balozi Isabella na wadau wengine ambao wameamua kuwajengea nyumba ya kisasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha lulanzi Lucas Kihongosi amewshukuru wadao hao wa maendeleo kwa kujitoa kuwasaidia walemavu hao huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza kwa wingi kuunga juhudi ambazo zimeanzishwa kwa kuchangia kupitia taasisi ya Isabella.
FEDHA zote zinapolokelewa kupitia acaount namba ya CRDB iliyosajiliwa kwa jina la Isabella African Foundation ya 015C621885600 huku Miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi Mei mpaka Julai 2022.