Familia ya watu wenye ulemavu Lulanzi Wilaya ya Kilolo wapatiwa Msaada wa Magodoro
11 May 2022, 3:53 am
Familia ya watu watatu wenye ulemavu katika kijiji cha Lulanzi Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa imekabidhiwa magodoro manne ya kitabibu na Balozi wa utalii Tanzania Bi Isabella Mwampamba akiwa na wadau wa maendeleo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi magodoro hayo, Bi Liliani Mbedule mdau wa maendeleo kwa watu wenye ulemavu amesema kuwa magodoro hayo yamegharimu kiasi shilingi milioni moja laki tatu na elfu sabini na nne na yamenunuliwa kwa ushirikano wa balozi Isabella, Familia ya Allan Kijazi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mh. Jastine Lazaro Nyamoga.
Aidha Bi Liliani amewaomba wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kuwasadia walemavu hao kwani bado wana uhitaji wa huduma za kijamii.
Kwa upande wake Balozi wa utalii Tanzania Isabella Mwampamba amesema kuwa huo ni muendelezo wa utalii wa kujitolea kwa kuwasaidia walemavu hao ambapo magodoro hayo yatawasaidia walemavu hao kulala sehemu salama na kuwapunguzia maumivu ya mgongo ambayo walikuwa wakiyapata kutokana na kulala sehemu ambayo siyo rafiki.
Naye Dada wa walemavu hao Pelaja Mpogole ameshukuru kwa kupatiw magodoro hayo kwani hapo wali ndugu zake walikuwa wanalala sehemu ambayo inawafanya wazidi kuumwa migongo.
“Kwa kweli niwashukuru sana Isabella na msafara wake kwa kutuletea magodoro haya kwani ndugu zangu walikuwa wanalala katika magodoro yaliyochakaa ambayo yalipelekea wao kuumwa mgongo, hivyo ujio wa msaada huu utawafanya ndugu zangu kulala sehemu bora” alisema Pelaja.
Lucas Kihongosi Ni Mwenyekiti wa Kijiji cha lulanzi, amewashukuru wadau hao waliojitokeza kuisaidia familia hiyo ya watu wenye ulemavu huku akiwataka wananchi kuendelea kuwasaidia ili waweze kuishi maisha yenye furaha.
Licha ya utoa msaada wa magodoro, Pia wamewapatia mahitaji ya kibinadamu mengine kama mchele, mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia na sukari.